Zenj FM

Hemed Suleiman kuongoza Kijini Shangwe 2026, maelfu watarajiwa kujumuika

11 September 2026, 18:41

Mwakilishi wa Jimbo la Kijini, Badria Attai Masoud, akizungumza na waandishi wa habari. Forodhaniu Zanzibar.

Bonanza la Kijini Shangwe 2026 linatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 3,500, likiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, kama mgeni rasmi. Tukio hilo litajumuisha michezo, matembezi ya kilomita 5, burudani na fursa za kiuchumi kwa wananchi, wakiwemo wanawake, vijana na wajasiriamali.

Na Mary Julius.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Bonanza la Kijini Shangwe 2026, linalotarajiwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya elfu tatu mia tano.

Bonanza hilo litafanyika Septemba 12 katika Jimbo la Kijini, Mkoa wa Kaskazini, likilenga kuimarisha umoja, mshikamano na afya kupitia michezo na shughuli za kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwakilishi wa Jimbo la Kijini, Badria Attai Masoud, amesema bonanza hilo litaanza kwa matembezi ya kilomita tano kuelekea uwanja mpya wa michezo wa Wilaya, kabla ya kufuatiwa na michezo mbalimbali ikiwemo mechi ya kirafiki kati ya Kijini na Mahonda.

Badria amesema bonanza hilo pia litakuwa jukwaa la wananchi kupata fursa za kiuchumi, ambapo vikundi tisa vya wanawake na kimoja cha vijana vitazinduliwa na kuwezeshwa kiuchumi.

Amesema wajasiriamali watapatiwa mitaji, wavuvi vifaa vya uvuvi, huku wananchi wakipata elimu na fursa za huduma mbalimbali, ikiwemo kujiunga na bima ya afya.

Sauti ya Mwakilishi wa Jimbo la Kijini, Badria Attai Masoud.
Vijana wa Makachu Forodhani wakiwa na Mwakilishi wa jimbo la Kijini Badria Attai Masoud,

Aidha, wajasiriamali watapata nafasi ya kuonesha na kuuza bidhaa zao, hatua inayolenga kuwaongezea masoko na kipato.