Zenj FM
Zenj FM
25 September 2026, 08:05

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, amezitaka Kamati za Maafa na Wataalamu kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na mvua za El Nino zinazotarajiwa. Ameagiza maeneo hatarishi, ikiwemo mabonde, mitaro na maeneo ya uchimbaji mchanga, kutambuliwa na kuchukuliwa hatua mapema.
NA Mwandishi wetu.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, amesema bado kuna kazi ya ziada kwa Kamati za Maafa na Kamati za Wataalamu za Wilaya mkoani humo katika kusimamia mikakati iliyowekwa kukabiliana na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha mwezi ujao.
Akizungumza na wajumbe wa kamati hizo mara baada ya kuwasilisha taarifa za mipango yao ya kukabiliana na hali hiyo, Hamida amesema ni wakati sasa kwa kamati hizo kutembelea maeneo yanayohofiwa kuathirika zaidi endapo mvua hizo zitanyesha kwa kiwango kilichotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Amesema hatua hiyo itasaidia kubaini mapema maeneo yenye changamoto, ikiwemo maeneo ya mabondeni, maeneo yanayochimbwa mchanga, mitaro inayoweza kuziba pamoja na maeneo yaliyo pembezoni mwa miundombinu ya barabara.
Aidha, amezitaka kamati hizo kusimamia masuala ya usafi, hususan katika maeneo ya dampo yasiyo rasmi, pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza.
Hamida amesisitiza umuhimu wa kamati hizo kushirikiana kikamilifu na mamlaka na taasisi zinazohusika na sekta zilizoainishwa kuwa na changamoto, ili changamoto hizo zipatiwe ufumbuzi wa pamoja kwa lengo la kunusuru maisha ya wananchi na kulinda mali zao.
Hata hivyo, amewataka viongozi wa Wilaya na Shehia kuendelea kuwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari, pamoja na kufuatilia taarifa rasmi zinazotolewa na Serikali na Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Wakitoa taarifa za kitaalamu kuhusu mikakati ya kukabiliana na maafa, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Kati, Mwanaisha Ali Said, na Mkurugenzi wa Baraza la Mji Kusini, Mussa Ali Mussa, wamesema taasisi zao tayari zimejipanga kutoa elimu kwa jamii kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa, ikiwemo kuhama katika maeneo hatarishi kama mabondeni na maeneo ya dago, kuchimba vyoo kwa baadhi ya kaya pamoja na kuweka akiba ya chakula.
Kwa upande wao, wajumbe wa kamati hizo wamesema, kutokana na umuhimu wa maandalizi ya mapema, kila mmoja kwa nafasi yake atawajibika kusimamia utekelezaji wa mikakati hiyo, ili kulinda maisha ya wananchi, mali zao pamoja na miundombinu ya Serikali na jamii.