Zenj FM
Zenj FM
10 November 2026, 21:09

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amezitaka nchi za Afrika kuwekeza katika Akili Unde na rasilimaliwatu ili kuboresha huduma za umma, huku APS-HRMNET ikitangaza kupata makao ya kudumu Dodoma. Mkutano huo wa Zanzibar umewakutanisha washiriki zaidi ya 1,000 kutoka nchi 21 za Afrika.
Na Mary Julius
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, amesema matumizi ya teknolojia ya Akili Unde yanapaswa kwenda sambamba na uwekezaji katika rasilimaliwatu ili kuongeza ufanisi wa Serikali na kuboresha huduma kwa wananchi.
Othman ameyasema hayo alipomwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 11 wa Mtandao wa Mameneja wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika (APS-HRMNET), uliofanyika Hoteli ya Verde, Zanzibar.
Amesema teknolojia pekee haiwezi kuleta maendeleo bila watumishi wenye maarifa, ujuzi na weledi, huku akizitaka Serikali za Afrika kuweka miongozo ya matumizi ya Akili Unde inayozingatia maadili, usalama wa taarifa na haki za wananchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema Akili Unde ina nafasi muhimu katika kuimarisha utendaji wa Serikali na kurahisisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za utoaji huduma kwa wananchi.
Naye Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo Zanzibar, Suleiman Masoud Makame, kwa niaba ya Waziri wa Katiba, Sheria, Utawala Bora na Utumishi wa Umma, Mwalimu Haroun Ali Suleiman, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya utumishi wa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Katika mkutano huo, Rais wa mtandao wa APS-HRMNET Xavier Mrope Daudi ametangaza kuwa mtandao huo umepata makao ya kudumu jijini Dodoma, baada ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutenga jengo maalumu kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Amesema makao hayo yatakuwa kituo cha uratibu, mafunzo na kujenga uwezo wa wataalamu wa rasilimaliwatu barani Afrika.
Naye Mwakilishi wa Chama cha Usimamizi wa Utawala wa Umma Afrika (APAM) Dkt John Nakabago amesisitiza kuwa Akili Unde isichukue nafasi ya utu na maadili ya binadamu, akitaka matumizi yake yaongozwe na uwajibikaji, uwazi na ulinzi wa taarifa za wananchi.
Amesema mageuzi ya utumishi wa umma yanahitaji kuwekeza kwa watumishi wenye ujuzi, uongozi bora na taasisi zinazoweka wananchi mbele, huku akiwaalika washiriki kuhudhuria Mkutano wa 45 wa Meza ya Mviringo ya APAM utakaofanyika Lesotho kuanzia Desemba 8 hadi 11.
Mkutano huo wa siku nne umewakutanisha zaidi ya washiriki 1,000 kutoka nchi 21 za Afrika, wakiwemo mawaziri, wataalamu na mameneja wa rasilimaliwatu, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya kuimarisha utumishi wa umma barani Afrika.
Mkutano huo una kaulimbiu isemayo: “Kuwezesha Mageuzi ya Kimkakati ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kwa Kutumia Akili Unde.”