Zenj FM
Zenj FM
28 October 2026, 18:40

Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Zanzibar kimeandika historia kwa kufanya mahafali yake ya kwanza, ambapo wanafunzi 188 wamehitimu, wakiwemo wanawake 127. Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa, amewataka wahitimu kuzingatia maadili, kujiajiri na kutumia elimu yao kuleta maendeleo, huku ujenzi wa kampasi hiyo ukiendelea kufungua fursa zaidi za elimu Zanzibar.
Na Mary Julius.
Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Khamis Mussa, amewataka wahitimu wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) kuzingatia maadili ya taaluma, kuwa waadilifu na kutumia elimu yao kujiajiri na kubuni fursa mpya za ajira.
Akizungumza katika Mahafali ya 24 ya TIA, ambayo ni ya kwanza kufanyika katika Kampasi ya Zanzibar, Balozi Mussa amewasisitiza wahitimu kutii sheria za nchi, kuepuka makundi yenye mienendo isiyofaa na kutumia teknolojia katika shughuli halali za kiuchumi.
Waziri Mussa amewapongeza wahitimu 188, wakiwemo wanawake 127, sawa na asilimia 67.6, akisema mafanikio hayo yanaonesha hatua katika kuimarisha usawa wa kijinsia katika elimu.
Aidha ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutoa ekari 60 kwa ajili ya ujenzi wa kampasi hiyo, ambao ujenzi umefikia asilimia 45. huku shilingi bilioni 30 zikitarajiwa kutumika mpaka kukamilika kwa ujenzi wa kampasi ya Makunduchi.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo, amesema kuanzishwa kwa Kampasi ya Zanzibar kumepunguza gharama za masomo kwa wanafunzi waliokuwa wakilazimika kusoma katika kampasi nyingine.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara, Jevonness Aikaeli, amesema bodi itaendelea kusimamia ubora wa elimu, uadilifu na mitaala inayoendana na mahitaji ya soko la ajira, ikiwemo uhasibu wa kimataifa na uchumi wa buluu.
Nao Baadhi ya wahitimu wameushukuru uongozi wa chuo kwa kuanzisha kampasi hiyo, wakisema imewarahisishia kupata elimu inayo tolewa na chuo hicho wakiwa Zanzibar na kupunguza gharama za masomo.