Zenj FM
Zenj FM
25 October 2026, 22:27

Usajili wa watu wenye ulemavu Zanzibar umeelezwa kuwa hatua muhimu ya kuwawezesha kutambuliwa, kupata haki zao na kunufaika na huduma pamoja na fursa za maendeleo. UWZ imehimiza jamii kushirikiana kuwahamasisha watu wenye ulemavu kujiunga na jumuiya husika ili kurahisisha upatikanaji wa huduma zinazostahili.
Na Mary Juliuss.
Usajili wa watu wenye ulemavu umeelezwa kuwa hatua muhimu katika kuhakikisha kundi hilo linatambuliwa, linasikilizwa na kupata haki pamoja na huduma zinazostahili.
Zoezi hilo linatarajiwa kusaidia kubaini changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu na kurahisisha upatikanaji wa fursa mbalimbali za maendeleo kupitia jumuiya za watu wenye ulemavu Zanzibar.
Akizungumza wakati wa zoezi la usajili lililofanyika katika Skuli ya Jumbi, Afisa kutoka Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, kitengo cha Wanachama, Mafunzo na Maendeleo, Fatma Juma Saidi, amesema baadhi ya shehia zimekuwa na uelewa mdogo kuhusu jumuiya za watu wenye ulemavu na umuhimu wake.
Amesema jumuiya hizo zina jukumu la kuwatambua watu wenye ulemavu, kufahamu changamoto zinazowakabili na kusaidia kutafuta ufumbuzi wa mahitaji yao.
Aidha, amesema kujiunga na jumuiya hizo kunaweza kuwawezesha kupata vitambulisho maalumu vinavyoweza kuwasaidia kunufaika na baadhi ya huduma, ikiwemo usafiri wa umma kwa kulipa nusu ya nauli, kwa mujibu wa utaratibu husika.
Fatma pia ameushukuru uongozi wa SHIJUWAZA kwa kuichagua Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu na kuifanya miongoni mwa mashirika ya watu wenye ulemavu (DPOs) yaliyoshiriki katika zoezi hilo, akieleza kuwa ushiriki huo umechangia kuwafikia watu wenye ulemavu kwa kiasi kikubwa Unguja na Pemba.
Kwa upande wake, Katibu wa Kikundi cha Watu Wenye Ulemavu cha Kijaruba, Jumbi, Ali Kombo Malim, amesema zoezi hilo litasaidia kuwatambua watu wenye ulemavu na kurahisisha usambazaji wa huduma zinazokidhi mahitaji yao.
Ameeleza kuwa usajili huo utawasaidia watu wenye ulemavu kufahamu haki zao na kupata taarifa kuhusu fursa mbalimbali, zikiwemo za usafiri na huduma nyingine zinazoweza kupatikana kupitia jumuiya zao.
Amewataka watu wenye ulemavu kutokata tamaa, bali kushiriki kikamilifu katika fursa mbalimbali zinazojitokeza ili kuboresha maisha yao na kujiletea maendeleo.
Naye Mtumwa Hamad Mjaka, kutoka Shehia ya Jumbi, amesema zoezi hilo limewapa faraja wazazi wa watoto wenye ulemavu, ambao baadhi yao wamekuwa wakikosa uelewa kuhusu mahali pa kuanzia na taratibu za kuwasajili watoto wao.
Ameiomba jamii kushirikiana katika kuwahamasisha wazazi na walezi kuwapeleka watoto wenye ulemavu katika jumuiya husika ili wasajiliwe, watambuliwe na waweze kupata haki pamoja na huduma zinazostahili.