Zenj FM
Zenj FM
20 October 2026, 23:15

Wanawake wanaongoza katika kilimo cha mwani Zanzibar, Serikali inalenga kuongeza thamani ya zao hilo kupitia teknolojia, usindikaji na uwekezaji. Je, mwani unaweza kuwa chanzo kikubwa zaidi cha kipato kwa wanawake na vijana? Waziri Shariff Ali Shariff aeleza mkakati huo.
Na Mary Julius.
Waziri wa Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, amesema Serikali ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi itaendelea kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu kwa kuwekeza katika teknolojia, utafiti, huduma kwa wakulima na usindikaji wa mwani ili kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi.
Waziri Shariff ameyasema hayo wakati akifungua jukwaa la majadiliano ya kitaalamu kuhusu Sera ya Mwani Zanzibar, lililofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr, Mbweni, amesema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan wanawake, ambao wanajumuisha sehemu kubwa ya wakulima wa mwani Zanzibar.
Ameeleza kuwa ni muhimu kujenga mfumo unaowawezesha wakulima kupata tija, masoko ya uhakika na kunufaika na mnyororo mzima wa thamani ya bidhaa za mwani.
Waziri huyo amesema soko lenye manufaa zaidi ni lile la bidhaa zilizotengenezwa kutokana na mwani, badala ya kuuza mwani ghafi pekee. Kwa mujibu wake, mwani unaosindikwa na kuongezewa thamani unaweza kuuzwa kwa bei ya juu na kuongeza kipato cha wakulima.
Amesema jukwaa hilo linalenga kujadili vivutio vinavyoweza kuwasaidia wakulima na wafanyabiashara, pamoja na kuweka mazingira yatakayowavutia vijana na wanawake zaidi kuingia katika sekta hiyo.
Aidha, waziri Shariff amesisitiza haja ya kuipa sekta ya mwani kipaumbele kwa kuongeza uwekezaji katika usindikaji, akibainisha kuwa chini ya asilimia 10 ya mwani unaozalishwa Zanzibar husindikwa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Zahor Kassim Al-kharous, amesema Zanzibar iliuza takribani tani 20,000 za mwani mkavu mwaka 2025, huku wanawake ambao ni miongoni mwa kundi kubwa linalojishughulisha na kilimo hicho, wakikadiriwa kufikia asilimia 90.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhan Mohammed, amesema taasisi hiyo iko tayari kuwawezesha wakulima, hususan wanawake, kuongeza thamani ya bidhaa zao ili kunufaika zaidi na fursa za kiuchumi zinazotokana na zao hilo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Amos Manyama, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kukuza teknolojia, uvumbuzi na uwekezaji ili kuongeza ushindani wa bidhaa za mwani katika masoko ya ndani na kimataifa.