Zenj FM

Zanzibar yaingia kwenye utalii wa kidijitali, vijana kunufaika na fursa mpya

13 October 2026, 17:36

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Dk. Nasra Nassor Omar, akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa JamboGo.Africa, Mohamed Hassan Mitawi, wakibonyeza kitufe kuashiria kuzinduliwa kwa JamboGO.Africa.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Dk. Nasra Nassor Omar, amesema jukwaa la kidijitali la JamboGo.Africa litafungua fursa mpya za ajira na biashara kwa kuwaunganisha watalii na watoa huduma mbalimbali. Amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia yatasaidia kutangaza vivutio vya Zanzibar kimataifa na kuwawezesha vijana na wajasiriamali kunufaika moja kwa moja na ukuaji wa sekta ya utalii.

Na Mary Julius.

WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Dk. Nasra Nassor Omar, amesema matumizi ya teknolojia ya kidijitali yatasaidia kukuza utalii, kuongeza ajira na kufungua fursa za biashara kwa wananchi, hususan vijana na wajasiriamali.

Amesema hayo wakati wa uzinduzi wa jukwaa la kidijitali la JamboGo.Africa uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Zanzibar.

Dk. Nasra amesema jukwaa hilo litawaunganisha watalii na watoa huduma mbalimbali, wakiwemo hoteli, waendeshaji wa utalii, wasanii, wabunifu na waandaaji wa matukio, huku likirahisisha upatikanaji wa taarifa na kutangaza vivutio vya Zanzibar katika masoko ya ndani na kimataifa.

Amesisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa hiyo kutangaza na kuuza bidhaa na huduma zao ili wanufaike moja kwa moja na ukuaji wa sekta ya utalii. Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuweka mazingira rafiki ya kisera na kisheria, huku ikizingatia ubora wa huduma, usalama wa taarifa na haki za watumiaji.

Sauti ya Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Dk. Nasra Nassor Omar.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa JamboGo.Africa, Mohamed Hassan Mitawi, amesema jukwaa hilo limeanzishwa ili kuwawezesha watoa huduma za utalii kutangaza biashara zao na kufikia masoko mapana zaidi.

Amesema mfumo huo utawawezesha watalii kupata huduma mbalimbali katika sehemu moja, zikiwemo hoteli, tiketi, mikahawa, usafiri, matukio na burudani, hatua inayolenga kurahisisha maandalizi ya safari na kuboresha uzoefu wa watalii.

Sauti ya Mkurugenzi Mkuu wa JamboGo.Africa, Mohamed Hassan Mitawi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI), Suleiman Ali Mohammed, amesema chama hicho kinaunga mkono uanzishwaji wa jukwaa hilo na kuitaka Serikali kushirikiana na wadau kuhakikisha linawanufaisha wawekezaji na watoa huduma wa utalii.

Sauti ya Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI), Suleiman Ali Mohammed.

Kwa upande wake, Biubwa Omar Khamis, kwa niaba ya Zanzibar National Chamber of Commerce (ZNCC), amesema JamboGo.Africa ni jukwaa linalolenga kuinua biashara za wazawa wa Afrika na kufungua fursa mpya za kiuchumi kupitia teknolojia ya kidijitali.

Sauti ya Biubwa Omar Khamis.