Zenj FM

Drone zazidi kuwapa wasiwasi wananchi ubago uwandani, wataka ufafanuzi wa serikali.

3 November 2026, 14:57

Eneo la ubago Uwandani.

Wananchi wa Ubago uwandani wameiomba Serikali kuweka wazi mipango ya matumizi ya ardhi zao na kuhakikisha tathmini na ulipaji wa fidia vinafanyika kwa haki, huku wakieleza kuishi kwa wasiwasi kwa takribani miaka minane. Serikali kupitia Mkuu wa Wilaya imewahakikishia wananchi kuwa watapewa ufafanuzi endapo maeneo yao yatahitajika kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Na Mary Julius,

Wananchi wa Ubago uwandani wameiomba Serikali kuweka wazi mipango ya matumizi ya maeneo yao yanayotajwa kuhitajika kwa uchimbaji wa vifusi kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara, wakitaka kufanyiwa tathmini ya haki na kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa ulipaji wa fidia.

Wakizungumza kuhusu suala hilo, wananchi hao wamesema wamekuwa katika hali ya sintofahamu kwa muda mrefu, huku baadhi yao wakidai kutoridhishwa na tathmini zilizofanyika na kiasi cha fidia kilicholipwa kwa baadhi ya wamiliki wa maeneo.

Sauti za Wananchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Wananchi inayoshughulikia migogoro ya ardhi, Ubago uwandani  Hassan Ramadhani Hassan, amesema wananchi hawapingi utekelezaji wa miradi ya maendeleo, bali wanahiaji uwazi wa serikali.juu ya maeneo hayo na tathmini kwa yale maeneo yanayohitajika.

Amesema kwa takribani miaka minane wananchi wamekuwa wakikabiliwa na zuio la kufanya shughuli za maendeleo na ujenzi katika maeneo wanayoishi, hali inayowaathiri kiuchumi na kijamii.

Ameongeza kuwa kupita kwa ndege zisizo na rubani (Drone) katika maeneo hayo kumezidisha wasiwasi wa wananchi kuhusu hatma ya makazi na maeneo yao.

Sauti ya Mwenyekiti wa Kamati ya Wananchi inayoshughulikia migogoro ya ardhi, Ubago uwandani  Hassan Ramadhani Hassan,

Akizungumzia suala la fidia, mkazi wa Ubago, Mohamed Issa Mcha, amesema baadhi ya wananchi hawajaridhishwa na kiasi cha fedha walicholipwa ikilinganishwa na ukubwa wa maeneo, nyumba na mimea iliyokuwemo.

Ametoa mfano wa eneo lenye nyumba na mimea ambalo yeye akiwa kama mmiliki wake amelipwa shilingi milioni 80, amesisitiza  umuhimu wa tathmini kuzingatia thamani halisi ya mali za wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya kati Rajabu Ali Rajabu amesema Serikali ina utaratibu wa kushughulikia maeneo yanayohitajika kwa ajili ya miradi ya maendeleo, akieleza kuwa endapo kampuni itahitaji eneo lolote, atakutana na wananchi husika ili kuwafahamisha na kueleza hatua zinazopaswa kufuatwa.

Mkuu wa Wilaya kati Rajab Ali Rajab,amewataka wananchi wenye malalamiko au wanaohisi kukumbwa na changamoto katika suala hilo kufika ofisini kwake ili kueleza matatizo yao na kupata ufafanuzi.

Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea na shughuli za ujenzi katika maeneo yao endapo hawajapewa zuio rasmi na Serikali au Mahakama.

Sauti ya Mkuu wa wilaya Kati.