Zenj FM
Zenj FM
9 October 2026, 21:38

Zanzibar inatarajia kupokea washiriki zaidi ya 800 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika katika Mkutano Mkuu wa Rasilimali Watu wa Sekta ya Umma, utakaajadili matumizi ya akili unde (AI) na mikakati ya kuboresha utendaji wa taasisi. Waziri Ridhiwani Kikwete amesema mkutano huo utakaofanyika Novemba 10, 2026, utatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na maarifa, huku ukilenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali watu na kukuza maendeleo barani Afrika.
Washiriki zaidi ya 800 wanatarajiwa kushiriki Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimali Watu katika Sekta ya Umma Barani Afrika, utakaofanyika Novemba 10 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Waziri Wanchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete amesema mkutano huo utawakutanisha wataalamu na wasimamizi wa rasilimali watu kutoka maeneo mbalimbali, afrika kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu mpya za kukabiliana na mabadiliko yanayoendelea katika sekta hiyo kwa lengo la kujadili mabadiliko ya kimkakati katika usimamizi wa rasilimali watu, hususan matumizi ya akili unde katika kipindi hiki cha mapinduzi ya kiteknolojia.
Amesema nchi kadhaa zimeonesha nia ya kushiriki mkutano huo, zikiwemo Tanzania Bara, Zanzibar, Namibia, Zimbabwe, Kenya na Uganda, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kujadili changamoto na fursa za usimamizi wa rasilimali watu barani Afrika.
Kikwete ameeleza kuwa mkutano huo utakuwa na mada tano zitakazowasilishwa na wataalamu, zikijikita katika mabadiliko ya kimkakati ya rasilimali watu, kukabiliana na maendeleo ya teknolojia na kutumia fursa za akili unde kuongeza ufanisi na kuimarisha utendaji wa taasisi za umma.
Aidha Amesisitiza kuwa maendeleo ya teknolojia yanahitaji wataalamu kujiimarisha kiujuzi ili kuendana na mabadiliko hayo na kuhakikisha akili unde inatumika kurahisisha utekelezaji wa majukumu na kuchochea maendeleo katika taasisi na nchi za Afrika.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Dkt. Haroun Ali Suleiman, amesema amani, umoja na utulivu vilivyopo Zanzibar ni miongoni mwa misingi muhimu inayowezesha kufanyika kwa mikutano mikubwa ya kimataifa na kuvutia washiriki kutoka mataifa mbalimbali.
Dkt. Suleiman amewataka wataalamu kuitumia teknolojia kama nyenzo ya kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi badala ya kuichukulia kama sababu ya kupunguza juhudi au kukwepa wajibu wao, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kujifunza, kujituma na kuwajibika.
Aidha, viongozi hao wameeleza umuhimu wa mikutano ya kimataifa katika kukuza ushirikiano, kubadilishana maarifa na kuitangaza Zanzibar kimataifa, ikiwemo kuimarisha mwonekano wa vivutio vyake vya utalii na kuchangia maendeleo ya uchumi.