Zenj FM
Zenj FM
13 November 2026, 22:07

Waziri Haroun Ali Suleiman amewataka wataalamu wa rasilimali watu barani Afrika kutumia maarifa waliyoyapata kuleta mabadiliko katika taasisi zao, huku akitangaza ufadhili wa masomo kwa washiriki kutoka Tanzania, Sierra Leone na Somalia. Mkutano wa 11 wa APS-HRMNet uliwakutanisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 18 kujadili maboresho ya utumishi wa umma na matumizi ya teknolojia ya Akili Bandia (AI).
Wataalamu wa rasilimali watu barani Afrika wametakiwa kutumia maarifa na ujuzi walioupata katika Mkutano wa 11 wa Mtandao wa Mameneja wa Rasilimali Watu wa Utumishi wa Umma Afrika (APS-HRMNet) kuleta mabadiliko chanya katika taasisi zao.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman, wakati akifunga rasmi mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Verde Zanzibar,ambapo waziri amewasisitiza washiriki umuhimu wa uwajibikaji, uadilifu, bidii na uzalendo katika utumishi wa umma.
Waziri Haroun amesema wataalamu hao wanapaswa kurejea katika nchi na taasisi zao na kuyafanyia kazi kwa vitendo mapendekezo ya mkutano huo badala ya kuishia katika majadiliano, ili kuboresha mifumo ya usimamizi na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi.
Amesema mkutano huo umefanikiwa kuwakutanisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 18, wakiwemo takribani mameneja na wataalamu 1,200 wa rasilimali watu na utawala, waliojadili namna ya kuboresha utendaji wa taasisi za umma, ikiwemo matumizi ya Akili Bandia (AI) katika kurahisisha shughuli za kiutawala na kuongeza ufanisi.
Katika hatua nyingine, Waziri Haroun ametangaza ufadhili wa masomo kwa washiriki wawili kutoka kila nchi ya Tanzania, Sierra Leone na Somalia, watakaopata fursa ya kuja Zanzibar kusomea masuala ya usimamizi na maendeleo ya rasilimali watu kupitia Taasisi ya Utumishi wa Umma Zanzibar na kutunukiwa shahada.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Ridhiwani Jakaya Kikwete amesisitiza umuhimu wa wataalamu wa rasilimali watu kubadilika katika usimamizi na utungaji wa sera pamoja na uendeshaji wa shughuli za utumishi wa umma, huku akitaka watumishi wa ngazi za chini kupewa nafasi za kuonyesha vipaji na uwezo wao.
Aidha amesema kutambuliwa kwa Zanzibar ndani ya mtandao huo kumeipa nafasi muhimu ya ushirikiano wa kitaaluma na kubadilishana uzoefu na mataifa mengine, huku washiriki wakipata fursa ya kuitambua Zanzibar kwa upana zaidi kupitia utalii, urithi wa utamaduni na ukarimu wake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtandao wa APS-HRMNet Xavier Mrope Daudi amewataka wataalamu hao kuwa vinara wa mabadiliko katika taasisi zao kwa kutumia weledi na uzoefu walioupata, akieleza kuwa maendeleo ya taasisi na bara la Afrika yanategemea kwa kiasi kikubwa mifumo imara ya usimamizi wa rasilimali watu.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ukarimu na ushirikiano mkubwa ilioutoa kwa washiriki, huku akisema kuchaguliwa tena kwa Kamati Tendaji kwa muhula wa pili ni ishara ya imani waliyopewa na wanachama, na kuahidi kuimarisha mtandao huo ili uwe mfano bora wa kuigwa barani Afrika.