Zenj FM
Zenj FM
23 October 2026, 18:36

Wizara ya Afya Zanzibar imeongeza wito wa uchunguzi wa mapema wa saratani ya matiti baada ya wagonjwa 115 kugundulika mwaka 2025/2026, huku asilimia 58 wakiwa katika hatua za juu za ugonjwa huo. Kupitia kampeni ya Pink October, Serikali na wadau wa afya wanahamasisha wananchi kutambua dalili za saratani na kutumia huduma za uchunguzi mapema ili kuimarisha matibabu na kuokoa maisha.
Na Mary Julius.
Wizara ya Afya Zanzibar imewataka wananchi kujitokeza kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti mapema ili kuongeza nafasi ya kupata matibabu yenye mafanikio.
Wito huo ameutoa kufuatia kugundulika kwa wagonjwa 115 wa saratani ya matiti Zanzibar katika mwaka 2025/2026, ambapo asilimia 58 wamebainika kuwa katika hatua za tatu na nne za ugonjwa huo.
Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema uchunguzi wa mapema husaidia kugundua ugonjwa huo kabla haujafikia hatua za juu.
Akitoa ujumbe wa kampeni ya Pink October huko Mnazimmoja, amesema kupitia mpango wa Beat Breast Cancer, zaidi ya watu elfu 29 wamefanyiwa uchunguzi kati ya zaidi ya laki mbili waliopatiwa elimu kuhusu saratani ya matiti.
Ameeleza kuwa dalili za ugonjwa huo ni pamoja na uvimbe kwenye titi au kwapani, mabadiliko ya umbo la titi na chuchu kutoa damu au majimaji yasiyo ya kawaida, akisisitiza kuwa saratani ya matiti inaweza kuwapata wanawake na wanaume.
Naye Mkurugenzi wa Mradi wa Kuzuia Saratani ya Matiti na Mlango wa Kizazi shirika la JHPIEGO Daktari Maryrose Giattas, amesema kampeni ya Pink October inalenga kuhamasisha jamii kuhusu mapambano dhidi ya saratani ya matiti na shingo ya kizazi, kwa kutoa elimu kuhusu kinga na umuhimu wa uchunguzi wa mapema.
Amesema saratani ya matiti ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wanawake Zanzibar, hivyo wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi kuhusu dalili za magonjwa hayo.
Aidha Daktari Giattas amewahimiza wananchi kutumia huduma za uchunguzi zinazopatikana katika vituo vya afya ili kubaini saratani katika hatua za awali na kupata matibabu kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya Zanzibar, Daktari Faiza Abassi, ameishukuru Jhpiego kwa kushirikiana na Serikali katika huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti na shingo ya kizazi.
Aidha amesema kupitia programu ya The Pfizer Breast Cancer Project, vituo 28 vimewezeshwa kufanya uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti, sambamba na kuimarishwa kwa huduma za maabara ya hospital ya Lumumba.