Zenj FM
Zenj FM
21 June 2026, 21:00

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja limekanusha taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu madai ya ubaguzi wa ajira katika kampuni zinazofanya kazi Zanzibar, likisema taarifa hizo si za kweli. Polisi wameeleza kuwa matumizi ya vitambulisho katika kampuni ya CRJE ni hatua ya kiusalama na wanaendelea kumtafuta aliyesambaza taarifa hiyo kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Na Omar Hassan.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja limekanusha taarifa za kuwepo kwa ubaguzi katika ajira za Makampuni, taarifa mbazo zimesambaa katika mitandao ya kijamii zikionesha vijana wakilalamikia kudaiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ili kupata ajira katika kampuni zinazofanya kazi maeneo ya Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari huko Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kusini Unguja Kaimu Kamanda wa Polisi katika Mkoa huo Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Khamis Lise Mwampelwa amesema taarifa zilizosambazwa si za kweli na wananchi wanapaswa kuzipuuza.
Amesema baada ya Jeshi la Polisi Kufanya uchunguzi limebaini kuwa kampuni ya CRJE inayojishughulisha na ukandarasi wa Majengo imeweka utaratibu wa kutumia vitambulisho kwa wafanyakazi wanaoingia katika eneo hilo ili kuimarisha usalama.
Kaimu kamanda huyo wa Polisi amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja kwa kushirikiana na taasisi nyengine linamtafuta aliyerusha taarifa hiyo yenye kuleta taharuki kwa jamii ili aweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.