Zenj FM

RC Hamida aagiza uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha Kibuteni

24 June 2026, 22:19

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis,akizungumza katika mkutano wa hadhara uliozikutanisha shehia za Kizimkazi Mkunguni, Dimbani na Kibuteni.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, ameagiza kufanyika uchunguzi kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Kamati ya Misitu ya Kibuteni ili kubaini ukweli wa malalamiko yaliyotolewa na wananchi. Aidha, amesisitiza umuhimu wa viongozi wa shehia kutambua mipaka na maeneo ya akiba ya serikali ili kuzuia migogoro na uvamizi wa ardhi.

Na Mwandishi wetu.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, ameitaka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar kushirikiana na Katibu Tawala wa Mkoa na Wilaya pamoja na timu za wakaguzi wa ndani kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Kamati ya Misitu ya Shehia ya Kibuteni.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliozikutanisha shehia za Kizimkazi Mkunguni, Dimbani na Kibuteni, katika muendelezo wa ziara zake za kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Wilaya ya Kusini, Mkuu huyo wa Mkoa amesema uchunguzi huo utasaidia kubaini ukweli wa tuhuma zilizotolewa na wananchi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Hamida pia amezungumzia suala la maeneo ya ardhi ya akiba yaliyotengwa na Serikali kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo, akisisitiza kuwa kila sheha anawajibu wa kuyatambua maeneo hayo pamoja na mipaka ya shehia zake ili kuzuia uvamizi unaoweza kusababisha migogoro ya ardhi.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis.

Wakati huo huo, maafisa mbalimbali wa Serikali wamefafanua baadhi ya malalamiko yaliyowasilishwa na wananchi katika mkutano huo. Daktari Dhamana wa Hospitali za Wilaya ya Kusini, Mohd Mtumwa Mnyimbi, amesema suala la utunzaji wa siri za wagonjwa linaendelea kuzingatiwa kwa mujibu wa maadili ya taaluma ya afya, huku akibainisha kuwa kutoa siri za mgonjwa ni kinyume cha maadili ya kazi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Baraza la Mji Kusini, Mussa Haji, amesema changamoto ya wananchi kutokata vibali vya ujenzi pamoja na kuendesha ujenzi holela bado inaendelea kujitokeza katika Wilaya ya Kusini, hali inayochangia kuvuruga mipango miji iliyowekwa na Serikali.

Sauti ya Mkurugenzi wa Baraza la Mji Kusini, Mussa Haji

Nao baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wameeleza kuwa pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana katika shehia zao, bado kuna changamoto mbalimbali zinazohitaji ufumbuzi wa haraka. Miongoni mwa changamoto hizo ni uwepo wa wajumbe wa muda mrefu katika baadhi ya kamati za shehia, uhaba wa madaktari katika Kituo cha Afya ya Mama na Mtoto cha Kizimkazi, uvamizi wa maeneo tengefu pamoja na kutotambuliwa kwa mipaka ya maeneo mbalimbali, hali inayochochea kuibuka kwa migogoro ya ardhi mara kwa mara.

Aidha Wananchi hao wameiomba Serikali kuendelea kusikiliza na kushughulikia kero zao kwa wakati ili kuimarisha maendeleo na ustawi wa jamii katika Wilaya ya Kusini.

Sauti za wananchi.