Wilaya ya Magharib B kufanya operation kukamata mifugo inayozurura ovyo
9 September 2024, 2:45 pm
Na Mary Julius
Mstahiki Meya Baraza la Manisapaa Wilaya ya Magharib B Khamis Hassan Haji amewataka Madiwani na Watendaji wa Manispaa ya Wilaya Magharibi B kusimamia masuala ya usafi katika maeneo yao kwa kuondoa majaa yasiyo rasmi pamoja na kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa mapato katika maeneo mbali mbali ya Wilaya hiyo.
Baraza la Manisapaa Wilaya Magharibi B limesema litaendesha operation mbali mbali ikiwemo kukamata ngombe wanaozurura ovyo katika maeneo mbali mbali hususani barabarani ya Fuoni.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Wilaya ya Magharibi B Mstahiki meya Baraza la Manisapaa Wilaya ya Magharib B Khamis Hassan Haji amewataka madiwani kila mmoja kusimamia maelekezo ya Serikali ikiwemo kuimarisha usafi wa mazingira pamoja na kutoa elimu kwa wanajamii katika maeneo yao kuhusu baadhi ya tabia za wafugaji wa ngombe na mbuzi kuwacha mifugo yao ikizurura .
Amesema Baraza la Manispaa kwa kushirikiana na ofisi ya Wilaya itaendesha operation hiyo na wanyama watakaokamatwa watafikishwa katika maeneo maalum yaliotengwa na Serikali , hivyo amewasihi wafugaji kufuata maelekezo yanayotolewa na maafisa mifugo wa Wilaya ili kuepuka usumbufu ikiwemo kuchukuliwa mifugo yao.
Nao Baadhi ya Madiwani wa Manispaa hiyo wamewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa baraza la Manispaa katika masuala ya usafi ikiwemo kuhifadhi taka katika maeneo yaliyotengwa na Manispaa pamoja na kuacha kujenga vipanda vya biashara katika maeneo ya akiba ya Barabara.