Zenj FM
Zenj FM
19 May 2026, 22:54

Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar Saada Mkuya Salimu amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto pamoja na huduma za afya ya msingi nchini. Serikali pia imepanga kuongeza ajira kwa wataalamu wa afya, kuboresha mifumo ya kidijitali na mazingira ya kazi kwa watumishi wa sekta hiyo.
Na Mary Julius.
Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar Dkt Saada Mkuya Salimu amesema Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, huduma za afya ya msingi, pamoja na kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.
Waziri Saada ameyasema hayo wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 amesema hivyo ni moja ya vipaumbele vikuu katika mwaka wa fedha huo kwa lengo la kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.
Aidha, waziri amesema wizara imepanga kuongeza ajira na mafunzo kwa wataalamu wa afya, kuimarisha mifumo ya kidijitali ya taarifa za afya, pamoja na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa sekta hiyo.
Katika upande wa miundombinu, Waziri Dkt Saada amesema Serikali itaendelea na ujenzi wa hospitali za mikoa Unguja na Pemba, Hospitali ya Saratani Binguni, Hospitali ya Rufaa na Kufundishia Binguni pamoja na ukarabati na upanuzi wa Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Aidha waziri Dkt Saada amesema Wizara ya afya itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya afya pamoja na kuimarisha huduma za kibingwa na kibobezi ili kupunguza rufaa za wagonjwa nje ya Zanzibar.
Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Afya imeomba kuidhinishiwa bajeti ya shilingi bilioni 405.89 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na utoaji wa huduma za afya nchini.
Akizungumza pembeni mwa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya afya Zanzibar Dkt Mngereza Mzee Miraji amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuongeza nguvu katika sekta ya afya kwa kuongeza bajeti kutoka shilingi milioni 368 hadi kufikia milioni 405, sawa na ongezeko la asilimia 10.3.
Aidha Dkt.mngereza amesema serikali inatarajia kujenga hospitali nne za mikoa ili kukamilisha mzunguko wa hospitali za rufaa Zanzibar.