Zenj FM
Zenj FM
28 July 2026, 12:08

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja limeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kushirikiana na wananchi kwa kushiriki katika zoezi la usafi wa mazingira katika Hospitali ya Wilaya ya Mwera Pongwe. Hatua hiyo imepongezwa na wananchi pamoja na uongozi wa hospitali.
Na Mary Julius.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja limeahidi kuendelea kushirikiana na wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii, likieleza kuwa jukumu lake halijaishia katika kulinda amani na usalama pekee, bali pia kushiriki kikamilifu katika shughuli zinazogusa maisha ya wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Daniel Emanuel Shillah, baada ya askari wa jeshi hilo kushiriki zoezi la usafi wa mazingira katika Hospitali ya Wilaya ya Mwera Pongwe.
Kamanda Shillah amesema Jeshi la Polisi linaamini kuwa usalama na maendeleo ya jamii huenda sambamba, hivyo limekuwa likishirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi, viongozi wa shehia pamoja na wananchi katika kutekeleza shughuli mbalimbali zenye manufaa kwa jamii.
Amesema jeshi hilo litaendelea kutekeleza kampeni za usafi wa mazingira, kutoa elimu ya ulinzi na usalama katika skuli na vyuo vikuu, pamoja na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu, wakiwemo wagonjwa waliolazwa hospitalini na wafungwa waliopo magerezani.
Aidha Kamanda Shillah ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni msingi wa kudumisha amani, usalama na ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake, Daktari Dhamana Msaidizi wa Hospitali ya Wilaya ya Mwera Pongwe, Dkt. Omar Makame Ali, amesema uongozi wa hospitali hiyo umefarijika na ujio wa Jeshi la Polisi Kusini Unguja kushiriki katika zoezi la usafi wa mazingira.
Amesema si mara ya kwanza kwa jeshi hilo kushirikiana na hospitali hiyo, akibainisha kuwa hatua hiyo inaonesha mshikamano mkubwa kati ya sekta ya afya na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuwatumikia wananchi.
Nao baadhi ya wagonjwa waliokuwa wakipata huduma hospitalini hapo wamepongeza hatua ya Jeshi la Polisi kushiriki katika usafi wa mazingira, wakisema imeonyesha taswira mpya ya askari kuwa ni sehemu ya jamii inayojali afya, ustawi na maendeleo ya wananchi.