Zenj FM
Zenj FM
16 May 2026, 22:47

Mkuu wa Wilaya ya Kati Rajab Ali Rajab amewataka madiwani wa Wilaya ya Kati kubuni vyanzo vipya vya mapato pamoja na kusimamia ukusanyaji wa mapato katika wadi zao ili kuongeza mapato ya Baraza la Manispaa Kati.
Na Hakika Mwinyi.
Madiwani wa Wilaya ya Kati wametakiwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ndani ya Baraza la Manispaa Kati pamoja na kufuatilia vibali vya ujenzi ili kufikia malengo walilojiwekea ya kuongeza mapato ndani ya Baraza hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kati Rajab Ali Rajab ameyasema hayo katika Kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa Kati, kikao cha robo ya tatu katika mwaka wa fedha 2025/2026 hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Uhamiaji Dunga Wilaya ya Kati Unguja.
Amesema Madiwani wanatakiwa kuhakikisha Wananchi wanalipa mapato kwa wakati ndani ya Wadi zao kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa ili kuweza kuanzisha vyanzo vipya vya mapato kupitia Wadi hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa Kati Dkt. Mwanaisha Ali Said amewaomba wananchi kutojenga katika hifadhi ya barabara na badala yake wafuate taratibu za ujenzi zinavyoelekeza ili kuepusha migogoro baina yao na Serikali.
Nae Mstahiki Meya wa Baraza hilo Said Hassan Shaaban amesema katika kipindi cha robo ya tatu Baraza limefanikiwa kujenga Vituo vya daladala vinne (4), pamoja na kumalizia ujenzi wa Bustani katika eneo la Hanyegwa Mchana .
Aidha Meya huyo amewaomba wananchi kuendelea kufuata taratibu zilizoekwa na Manispaa Kati hususani kuepuka ujenzi holela katika hifadhi za Barabara.