Zenj FM
Zenj FM
1 January 2026, 10:26 am

Na Mary Julius.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeida Rashid Abdalla, amewaomba viongozi wa wizara na taasisi mbalimbali za serikali kutambua wajibu wao wa kusaidia nchi katika mchakato wa kuridhia Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Watu Wenye Ulemavu.
Katibu Mkuu Abeida ametoa ombi hilo wakati akifungua kikao cha wakurugenzi kutoka wizara mbalimbali, kilicholenga kujadili Itifaki ya Afrika kuhusu haki za watu wenye ulemavu, uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Tume ya Uchaguzi, Magharibi B, Mazizini Zanzibar.
Amesema masuala ya watu wenye ulemavu ni masuala mtambuka, hivyo yanapaswa kuzingatiwa katika mipango, sera na programu za wizara na taasisi zote za serikali.
Aidha, amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kusimamia na kuthamini masuala ya watu wenye ulemavu, akibainisha kuwa wakati wa kampeni aliweka nafasi maalum kwa kundi hilo na ni mlezi wa watu wenye ulemavu.
Amehimiza wadau kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni na ushauri ili kuhakikisha itifaki hiyo inapitishwa Tanzania na masuala ya watu wenye ulemavu yanajumuishwa kikamilifu katika taasisi wanazozisimamia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar UWZ Abdulwakili H. Hafidhi, amesema kikao hicho kimelenga kujenga mashirikiano na kuwaongezea uelewa wadau kuhusu itifaki hiyo, ili wawe mabalozi wa kuisukuma mbele hadi kufanikisha kuridhiwa kwake na nchi.
Naye Afisa Mipango wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Suleiman Ali Hamad, amesema wizara hiyo imeipokea vizuri itifaki hiyo na kuahidi kuifanyia kazi, huku akisisitiza kuwa katika maandalizi ya mipango yao watahakikisha watu wenye ulemavu wanajumuishwa kama wanufaika wakuu wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti kutoka Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Ilyasa Pakacha Haji, amesema kuna haja ya kuendelea kuwajengea uelewa makatibu wakuu na mawaziri kuhusu mikataba ya kimataifa, hususan inayohusu watu wenye ulemavu.
Amesisitiza umuhimu wa kutumia sensa ya watu na makazi pamoja na kushirikiana na masheha ili kupata takwimu sahihi za watu wenye ulemavu katika shehia zao, jambo litakalosaidia kupanga mipango bora ya kuwawezesha.