Zenj FM
Zenj FM
4 June 2026, 17:20

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar imejipanga kuwa kitovu cha uwekezaji Afrika Mashariki kutokana na mazingira bora ya biashara, sera thabiti na miundombinu ya kisasa. Akifungua Jukwaa la Uwekezaji Zanzibar 2026 lililowakutanisha zaidi ya washiriki 700, amesema serikali imeweka mazingira salama na rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje.
Na Mary Julius.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar imejipanga kuwa moja ya maeneo bora zaidi ya uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kutegemea uthabiti wa sera, miundombinu ya kisasa, nguvu kazi ya vijana, nafasi ya kimkakati na ushirikiano wa karibu kati ya serikali na sekta binafsi.
Akifungua Jukwaa la Uwekezaji Zanzibar 2026 lililofanyika katika hotel ya Golden Tulip uwanja wa Ndege na kukutanisha washiriki zaidi ya 700 kutoka ndani na nje ya Tanzania, Rais Dk. Mwinyi amesema serikali imeweka mazingira salama na rafiki kwa wawekezaji ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu.
Rais Dk Mwinyi amesema maboresho ya miundombinu ikiwemo viwanja vya ndege, bandari za kisasa, barabara na uzalishaji wa umeme yanaifanya Zanzibar kuwa lango muhimu la biashara na usafirishaji katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Akizungumzia kaulimbiu ya jukwaa hilo ya “Kukuza Uwekezaji, Utofautishaji na Maendeleo Endelevu Zanzibar: Kuunda Hadithi Mpya ya Ukuaji wa Zanzibar”, Rais Dk. Mwinyi amesema serikali imeamua kwa makusudi kupanua vyanzo vya uchumi ili kupunguza utegemezi wa sekta moja.
Rais Dkt Mwinyi ameyataja maeneo yenye fursa kubwa ni pamoja na uchumi wa buluu, usindikaji wa mazao, nishati mbadala, viwanda, uvuvi, huduma za kidijitali na utalii wa kiwango cha kimataifa.
Kwa upande wake Waziri Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, amesema jukwaa hilo linalenga kujenga ushirikiano wa muda mrefu utakaosaidia kuharakisha maendeleo ya viwanda, upanuzi wa miundombinu, ukuaji wa utalii, mabadiliko ya kidijitali na uwekezaji katika nishati mbadala.
Neye,Mkurugenzi wa Zanzibar Investment Promotion Authority, Saleh Saad Mohamed, amesema taasisi hiyo itaendelea kutoa huduma bora kwa wawekezaji kupitia mfumo wa kituo kimoja na usaidizi wa sera.
Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM), Azana Hassan Msingiri, amesema taasisi hiyo itaendelea kuimarisha ulinzi wa mipaka ya bahari, miundombinu ya pwani na maeneo ya mazalia ya samaki ili kuhakikisha mazingira salama kwa uwekezaji na shughuli za uchumi wa buluu.
Kwa niaba ya wawekezaji, Jerry Tomath kutoka kampuni ya CRJE amesema mazingira mazuri ya biashara yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yamechangia kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta ya ujenzi na utoaji wa ajira kwa vijana.
Amesema sheria na sera zinazolinda uwekezaji zimewapa wawekezaji uhakika na utulivu wa kufanya kazi kwa ufanisi.