Zenj FM
Zenj FM
6 July 2026, 17:09

Mlundikano wa taka katika eneo la Nyerere, Wilaya ya Mjini, umeibua hofu ya kuongezeka kwa magonjwa kutokana na harufu mbaya na nzi wengi wanaozunguka maeneo ya makazi. Wananchi wameiomba Manispaa kuongeza kasi ya ukusanyaji wa taka na Serikali kutafuta suluhisho la kudumu kwa kujenga dampo jipya.
Na Safia na Mariam.
Wananchi wa eneo la Nyerere, Wilaya ya Mjini, wameiomba Manispaa kuongeza juhudi za kuhakikisha taka zinaondolewa mara kwa mara kabla hazijaanza kusababisha athari kwa wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya kutupia taka.
Wametoa ombi hilo wakati wafanyakazi wa Manispaa walipofika eneo hilo kuendelea na shughuli za ukusanyaji wa taka.
Wananchi hao wamesema kuchelewa kwa huduma ya kuondoa taka kunasababisha kuongezeka kwa nzi wengi, harufu mbaya, pamoja na hatari ya kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko yanayotokana na mazingira yasiyo safi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Sheha, Makame Kilindi Vuai, amesema kuwa ongezeko la taka katika eneo hilo linatokana na kutotosheleza kwa dampo lililopo, hali inayosababisha kujaa kwa haraka na kukosekana sehemu nyingine ya kutupia taka.
Ameiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa dampo jingine ili kuondoa tatizo la wananchi kutupa taka katika maeneo yasiyo rasmi, ambayo huleta usumbufu na kuhatarisha afya za wakazi wa karibu.
Naye Msimamizi Mkuu wa Masuala ya Usafi na Taka, Iklima Jumanne Khamisi, amesema Manispaa Mjini inaendelea kutekeleza jukumu la kuondoa taka katika Wilaya ya Mjini kwa lengo la kupunguza kero zinazowakabili wananchi.
Amewahakikishia wananchi kuwa jitihada zinaendelea kuimarishwa, ikiwemo kuandaa mfumo wa kujenga madampo ya kisasa yatakayosaidia kuboresha usimamizi wa taka na kuondoa changamoto zinazojitokeza katika maeneo mbalimbali.