Zenj FM
Zenj FM
22 July 2026, 20:43

Kutoka darasani hadi barazani, Maryam Said Khamis ametimiza ndoto yake ya uongozi kwa kuvuka kutoka taaluma ya ualimu hadi kuwa Mwakilishi na Mbunge, akitumia nafasi yake kuwatumikia na kuwawezesha wanawake pamoja na jamii. Safari yake inaonesha kuwa elimu, bidii na kutokata tamaa vinaweza kumfikisha mwanamke katika nafasi za juu za maamuzi na kuwa chachu ya mabadiliko kwa wengine
Na, Is haka Mohamed Rubea .
Ndoto ya kuwa kiongozi haikuanza pale alipoingia katika ulimwengu wa siasa, bali ilianza miaka mingi
iliyopita akiwa mwalimu darasani. Wakati wengine walimwona kama mfundishaji wa watoto, yeye aliona
ndani yake uwezo wa kufanya zaidi, kushiriki katika maamuzi na kuwa sehemu ya mabadiliko katika jamii
yake.
Hii ndiyo safari ya Maryam Said Khamis, mwanamke kutoka Kijiji cha Mikarafuuni, Shehia ya Ng’ombeni,
Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, ambaye leo anasimama kama mfano wa mwanamke
aliyethubutu kuishi ndani ya ndoto zake za kuwa kiongozi.
Maryam ni Mwakilishi wa Viti Maalum Wanawake kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Kusini
Pemba, na pia ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia nafasi ya uteuzi
kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa kipindi cha mwaka 2025 hadi 2030.
Safari yake ya uongozi inaonesha namna taaluma ya ualimu ilivyokuwa msingi wa kumpa uzoefu,
nidhamu na uwezo wa kuwatumikia wananchi katika ngazi kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Shehia ya Ng’ombeni alikozaliwa Maryam ina
jumla ya wakazi 3,711, ambapo wanaume ni 1,739 na wanawake ni 1,972, ikiwa na jumla ya kaya 726.
Mkoa wa Kusini Pemba una jumla ya wakazi 271,350.
Maryam alianza elimu yake ya awali katika kijiji hicho kabla ya kuendelea na masomo ya sekondari
Uweleni. Baada ya kumaliza kidato cha sita, alijiendeleza katika taaluma ya ualimu na baadaye kuanza
kazi ya kufundisha mwaka 2002 huko Wesha kabla ya kuendelea na kituo cha Pondeani Chake Chake.
Akiwa mwalimu, Maryam hakuishia kwenye majukumu ya darasani pekee. Alianza kujenga uwezo wa
uongozi kupitia nafasi mbalimbali alizoshika huku akiwa na lengo la siku moja kufikia nafasi ya juu zaidi
katika kuitumikia jamii.
“Nilikuwa nasomesha lakini nilijiwekea malengo ya kuwa kiongozi. Nilitamani kufikia hatua ambayo
ningeweza kuheshimiwa na kuitumikia jamii yangu kwa nafasi kubwa zaidi. Hata nikiwa mwalimu
nilionesha nia hiyo kwa kushika nafasi mbalimbali za uongozi,” anasema Maryam.
Kutokana na utendaji wake na kujituma katika kazi, alipokea pongezi mbalimbali na baadaye
kuhamishiwa wizarani ambako aliendelea kuhudumu kwa miaka minne.
Mapenzi ya Siasa Yaliyomfikisha Barazani
Mbali na taaluma yake, Maryam alikuwa na mapenzi makubwa na siasa. Alianza kushiriki katika shughuli
za kisiasa akiwa na dhamira ya kuhakikisha wanawake wanapata nafasi zaidi katika uongozi na maamuzi.
Mwaka 2015 na mwaka 2020 alijaribu kuwania nafasi ya uwakilishi wa viti maalum wanawake wasomi
kupitia Chama cha Mapinduzi CCM. Katika hatua hiyo alipata kura 103, lakini hakufanikiwa kupata nafasi
kutokana na kutokidhi baadhi ya sifa zilizohitajika wakati huo.
Pamoja na changamoto hiyo, hakukata tamaa. Badala yake, aliitumia kama hatua ya kujifunza na
kuendelea kujiendeleza kielimu na kiuongozi.
“Nafasi hiyo ilikuwa ya kipekee iliyokuja Kusini Pemba lakini kwa utumishi ilikuwa kwa Pemba nzima.
Nilipata kura nyingi lakini nilikosa kutokana na sifa zilizohitajika wakati huo. Hilo lilinipa nguvu ya
kuendelea kujijenga zaidi kielimu,” anasema.
Baada ya miaka ya juhudi na maandalizi, mwaka 2025 Maryam alifanikiwa kupata nafasi ya uwakilishi wa
viti maalum wanawake Mkoa wa Kusini Pemba.
“Nawashukuru wote walioniunga mkono na kuniamini. Ninaahidi kuitumikia nafasi hii kwa maslahi ya wanawake wote wa Mkoa wa Kusini Pemba,” anasema.
Kiongozi anayegusa maisha ya wanawake
Tangu kuingia katika nafasi ya uwakilishi, Maryam ameanza kushughulikia changamoto zinazowakabili
wanawake na wananchi kwa ujumla.
Miongoni mwa juhudi zake ni kuwawezesha wanawake wajasiriamali wanaofanya biashara ndogo ndogo
kwa kuwapatia vifaa vya kufanyia kazi ikiwemo miavuli. Pia amesaidia wanawake wanaojishughulisha na
uchimbaji wa kokoto kwa kuwapatia nyundo na vifaa vingine vya kazi.
Aidha, amekuwa akitoa msaada kwa vikundi vya wanawake kupitia mitaji midogo midogo, kusaidia
wanafunzi katika kambi za masomo na kushirikiana na jamii kutafuta suluhisho la changamoto
mbalimbali.
“Nimeshaanza kushuka mtaa kwa mtaa, kijiji kwa kijiji, kusikiliza changamoto za kina mama na nimeanza kuzitafutia ufumbuzi,” anasema.
Kutoka utumishi wa umma hadi nafasi ya Katibu Tawala
Kabla ya kuingia katika uongozi wa kisiasa, Maryam aliendelea kujenga uzoefu katika utumishi wa
umma. Baada ya kuhudumu Wizara ya Biashara, aliteuliwa na Rais wa Zanzibar kuwa Katibu Tawala wa
Wilaya ya Kaskazini A Unguja.
Nafasi ya Katibu Tawala ni nafasi ya kiutawala inayohitaji uzoefu mkubwa katika uongozi na utumishi wa
umma. Katibu Tawala ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za kiutawala katika eneo husika, akiratibu
utekelezaji wa sera na maamuzi ya serikali, kusimamia watumishi wa umma na kuhakikisha huduma
zinatolewa kwa ufanisi.
Kwa kawaida, nafasi hiyo hupewa viongozi wenye elimu ya juu, uzoefu wa utawala, uadilifu, uwajibikaji
na uwezo wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia sheria na sera za serikali.
Familia na jamii wamshuhudia kama mwanamke mwenye maono
Muhammed Ayoub Muhammed, ambaye amekuwa karibu na Maryam tangu akiwa mwalimu Pondeani,
anasema mafanikio yake yametokana na uthubutu, uvumilivu na uwezo wake wa kufuatilia jambo
mpaka kulifikisha mwisho.
“Ukiacha ukarimu wake, Maryam ana tabia njema, bidii katika kazi na utayari wa kuongoza jamii.
Akiamua jambo analifuatilia mpaka litimie,” anasema.
Kwa upande wake, Zuwena Abdalla Haji, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania UWT Mkoa wa
Kusini Pemba, anasema Maryam ameonesha kujitoa katika kuwatumikia wanawake kwa kushughulikia
changamoto mbalimbali ikiwemo maji, afya, elimu na kuwawezesha wajasiriamali wadogo.
Anasema mafanikio ya Maryam ni matokeo ya kupenda ndoto zake na kufanya kazi kwa bidii ili kuzifikia.
Salma Muhammed, ambaye ni jirani yake, anaeleza kuwa huruma, imani, kujituma na kutokata tamaa ni
baadhi ya sifa zilizomfikisha Maryam katika nafasi hiyo.
Anasema safari yake ni funzo kwa wanawake wengine wenye malengo ya kuingia katika uongozi.
Wanawake katika Nafasi za juu za utawala Zanzibar
Kwa sasa Zanzibar ina jumla ya Makatibu Tawala 16 ambapo watano ni Makatibu Tawala wa Mikoa na
11 ni Makatibu Tawala wa Wilaya, Kati ya hao, wanawake hawajazidi usawa wa 50 kwa 50 wanakisiwa
kuwa ni 4 .
Hali hii inaonesha kuwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi unaendelea kuongezeka, ingawa
bado kuna nafasi ya kuongeza idadi yao.
Safari ya Maryam Said Khamis kutoka darasani hadi barazani ni ushahidi kuwa mwanamke mwenye
ndoto, elimu, ujasiri na dhamira anaweza kufikia nafasi kubwa za uongozi.
Leo, yeye si mwanamke aliyefanikisha ndoto zake pekee, bali ni mwanga na faraja kwa wanawake
wengine wanaotamani kuingia katika ulimwengu wa uongozi.
na ndivyo ambavyo wadau wa maswala ya wanawake na uongozi Zanzibar ambao ni Chama cha
waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA ZNZ wanavyoendelea kuziibua sauti za wanawake
viongozi ,na wanawake vijana na wanawake wnye ulemavu kupitia Program ya SWIL ambao ni chachu
ya maendeleo kama ambavyo Amina Ahmed Mohd Kaimu mratibu wa TAMWA upande wa Pemba
anavyosema juhudi na hatua kubwa zimefikiwa tangia kuongeza nuguvu za kuibua sauti za wanawake
kutafuta uongozi katika Nyanja za siasa democrasia na uchumi, kuna mabadiliko makubwa tulipotoka na
tulipofikia katika suala hili.
‘’ Tangia TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na PEGAO,JUWAUZA, NA ZAFELA katika kutafua usawa wa
kijinsia katika vyombo vya kutolea maamuzi kwenye teuzi mbali mbali tumepiga hatua na kufikia
asilimia 47 ya uongozi kwa wanawake na tunaamini kila siku zikienda juhudi zinaonekana na
mabadiliko yanapatikana.