Zenj FM

Miaka 6 ya ushirikiano, majeshi ya EAC yatoa matibabu bure kwa watoto Zanzibar

26 August 2026, 15:37

Daktari kutoka Jeshi la Uganda, Dkt. Fred Kyekulidde akimsikiliza mzazi katika kambi ya matibabu ya watoto SOS Mombasa Zanzibar.

Maadhimisho ya miaka sita ya ushirikiano kati ya majeshi ya Afrika Mashariki na wananchi yanaambatana na kambi ya matibabu bure kwa watoto Zanzibar. Kambi hiyo, iliyoandaliwa na Jeshi la Wananchi Tanzania kwa kushirikiana na majeshi ya Afrika Mashariki, inalenga kuwapatia watoto huduma za afya, ushauri wa kitabibu na dawa bila malipo.

Na Mary Julius.

Jeshi la Wananchi Tanzania kwa kushirikiana na majeshi ya Afrika Mashariki limeanza kambi ya matibabu ya bure kwa watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 14 katika viwanja vya SOS Children’s Village Zanzibar.

Akizungumza katika ufunguzi wa kambi hiyo Mkurugenzi wa Kijiji cha SOS Zanzibar, Asha Salim Ali, ametoa wito kwa skuli na jamii kuwapeleka watoto katika kambi ya matibabu inayofanyika katika viwanja vya SOS Children’s Village Zanzibar. Asha amesema zoezi hilo limeandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kushirikiana na majeshi mengine ya Afrika Mashariki, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka sita ya ushirikiano kati ya majeshi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na wananchi.

Amesema lengo kubwa ni kuhakikisha watoto wengi zaidi Zanzibar wanapata huduma za matibabu, ushauri wa kitabibu pamoja na dawa bila malipo.

Aidha, ameliipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kuandaa kambi hiyo, akisema hatua hiyo inalifanya Jeshi kuwa karibu zaidi na jamii na kuimarisha ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Sauti ya Mkurugenzi wa Kijiji cha SOS Zanzibar, Asha Salim Ali,

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Watoto kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Dkt. Clement Shija Hosea, amesema kituo cha SOS kinatoa huduma mbalimbali za afya kwa watoto, huku madaktari kutoka Uganda wakishiriki kutoa huduma za kibingwa.

Amesema miongoni mwa changamoto za kiafya walizokutana nazo ni magonjwa ya mfumo wa hewa, matatizo ya meno pamoja na macho.

Dkt. Clement amesema madaktari hao wamejipanga kuwafikia na kuwahudumia watoto wengi zaidi, huku dawa zikitolewa kwa watoto wanaohitaji matibabu.

Sauti ya Daktari Bingwa wa Watoto kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Dkt. Clement Shija Hosea

Naye Daktari kutoka Jeshi la Uganda, Dkt. Fred Kyekulidde, amesema kambi hiyo itasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya majeshi na wananchi, huku akisisitiza kuwa madaktari wamejipanga kuhakikisha watoto wanapata huduma bora za afya.

Sauti ya Daktari kutoka Jeshi la Uganda, Dkt. Fred Kyekulidde.

Kwa upande wao, watoto na walimu waliofika katika kambi hiyo wamepongeza huduma zinazotolewa, huku wakiiomba jamii kujitokeza kwa wingi kuwapeleka watoto kupata huduma.

Wamesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha afya za watoto na kuhakikisha changamoto mbalimbali za kiafya zinabainika na kutibiwa mapema.

Sauti ya Mwalimu na Wanafunzi.

Aidha, wamewashukuru wanajeshi kwa kuwatambua watoto kama sehemu muhimu ya jamii na kuwaandalia kambi hiyo ya matibabu.

Sauti ya Mzazi.

Kambi hiyo imeanza leo, Agosti 26, na inatarajiwa kumalizika Agosti 31.