Zenj FM

Maboresho ya afya Zanzibar yaleta furaha kwa wagonjwa na familia zao

11 June 2026, 14:44

Picha ya Hospital ya Jitimai.

Wananchi wa Zanzibar wamepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Nane kwa kusogeza huduma za afya za kibingwa katika hospitali za wilaya, hatua iliyopunguza gharama na usumbufu wa kusafiri nje ya visiwa kwa matibabu.

Na Mary Julius.

Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi imeendelea kusogeza huduma za afya za kibingwa karibu na wananchi kupitia hospitali za wilaya zilizopo Unguja na Pemba.

Hayo yameelezwa na baadhi ya wananchi walionufaika na huduma za kibingwa zinazotolewa katika Hospitali za Wilaya za Jitimai na Mbuzini, ambapo wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na uongozi wa hospitali hizo kwa kuimarisha huduma ambazo hapo awali zilipatikana katika hospitali za rufaa nje ya Zanzibar.

Akizungumza na Zenji FM, mmoja wa wanufaika wa huduma hizo amesema maboresho ya sekta ya afya yamewawezesha wananchi kupata matibabu ya kibingwa visiwani Zanzibar bila kulazimika kusafiri kwenda Tanzania Bara.

Aidha, mwanafamilia wa mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji maalumu amepongeza juhudi za madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo, hususan Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Shabbier Adamjee, akisema huduma hiyo imesaidia kurejesha matumaini na furaha kwa familia yao.

Sauti Mwananchi

Kwa upande wake, baba wa mtoto mwenye ugonjwa wa hemofilia amesema mtoto wake amekuwa akiishi na ugonjwa huo tangu kuzaliwa na sasa ana umri wa miaka 18. Ameeleza kuwa kwa muda mrefu familia yake ilikuwa ikigharamia safari za kufuatilia matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jambo lililokuwa likiwaongezea mzigo mkubwa wa kifedha.

Amesema kutokana na ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na uongozi wa Sefii Hospitali  Zanzibar, huduma hizo sasa zinapatikana visiwani Zanzibar, hatua iliyopunguza gharama na usumbufu wa safari kwa wagonjwa na familia zao.

Sauti ya Mzazi.

Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Shabbier Adamjee, amesema hospitali inaendelea kutoa huduma za kibingwa kwa viwango vya juu ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu bora karibu na maeneo yao bila ulazima wa kusafiri umbali mrefu.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano wa wataalamu wa afya pamoja na matumizi ya vifaa tiba vya kisasa vinavyowezesha utoaji wa huduma salama, bora na zenye kukidhi mahitaji ya wananchi.

Sauti ya Daktari Bingwa wa Upasuaji, Dkt. Shabbier Adamjee.