Adhabu kali atakayetumia mifuko ya plastik Zanzibar
3 October 2024, 3:56 pm
Na Khalida Abdulrahman na Jesca Pendael.
Jamii visiwani Zanzibar imetakiwa kuacha kutumia mifuko ya plastik ili kuepukana na uchafuzi wa mazingira, uharibifu wa ardhi pamoja na vifo vya wanyama kama ng’ombe na mbuzi.
Akizungumza na Zenj FM, Afisa wa Mazingira Hamdu Ibrahim Makame huko ofisini kwake Idara ya Mazingira Maruhubi Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Amesema Zanzibar ni kisiwa mojawapo kilichopiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki kupitia kifungu 22 (1) (E) cha sheria ya usimamizi wa mazingira namba 3 ya mwaka 2015 na kueleza kuwa yeyote atakayeingiza, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki atatozwa faini ya shilingi milioni moja au kufungwa kwa miezi mitatu na isiyozidi mwaka mmoja.
Aidha amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira imechukua jitihada kwa kuunda kitengo cha doria ili kuhakikisha sheria inafanyiwa kazi na kutoa elimu kwa jamii juu ya vifo vya wanyama na uchafuzi wa haiba ya ya kisiwa cha zanzibar.
Zenji FM ilipata wasaha wa kuzungumza na baadhi ya wananchi ambao wamezungumzia madhara ya matumizi ya mifuko ya plastiki ikiwa ni pamoja na ardhini kukosa rutuba ambapo kunasababisha kukosekana kwa chakula cha kutosha kwa binadamu.
Aidha wameishauri Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii juu ya madhara yatokanayo na matumizi ya mifuko ya plastiki kwani mifuko hiyo inaathiri afya za binadamu na ni moja wapo ya sababu ya kuongezeka kwa maradhi yasiyo ambukiza kama kansa.