Zenj FM
Zenj FM
17 April 2026, 3:33 pm

Jeshi la Polisi Zanzibar limeripoti kupungua kwa makosa ya udhalilishaji kwa asilimia 32.1 kutoka mwaka 2024 hadi 2025. Mafanikio hayo yanachangiwa na ushirikiano kati ya Polisi, Ofisi ya Mufti Mkuu, na programu ya “Usalama Wetu Kwanza” mashuleni.
Na Mary Julius.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Ulinzi wa mtoto Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, Mrakibu msaidizi wa Polisi Ali Mohd Othman amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na taasisi nyingne limefanikiwa kupunguza makosa ya udhalilishaji katika jamii kwa asilimia 32.1 ukilinganisha na mwaka 2024 – 2025 ambapo jumla ya makosa 1809 yaliripotiwa mwaka 2024 na makosa 1228 yaliripotiwa mwaka 2025.
Ameyasema hayo lipokuwa katika kikao maaluum cha mikakati ya kupambana na makosa ya udhalilishaji katika ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar huko Mazizini Mkoa wa Mjini Magharib, amesea kupungua kwa makosa hayo ni kutokana na ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Polisi na taasisi mbalimbali ikiwemo ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, pamoja na programu mbalimbali ambazo zimeanzishwa na Jeshi la Polisi ikiwemo somo la Usalama wetu kwanza katika skuli za msingi zilizopo Zanzibar.
Amesema Jeshi la Polisi kupitia Program yake ya Usalama wetu kwanza mashuleni imefanikiwa kurejesha wanafunzi zaidi ya 452 ambao walikua watoro na tayari wameshaacha skuli na kujiingiza katika vikundi visivyofaa.
Mrakibu huyo ameeleza kuwa pamoja na mafanikio hayo bado makosa hayo yanaendelea kutokea hivyo jamii inatakiwa ipatiwe elimu hasa ya kiroho katika kuzuia na kukabiliana na makosa hayo yasiendelee kutokea.
Kwa upande wake Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi amesema suala hili ni la kila mmoja katika jamii hivyo, ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar itaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi na kuhakikisha inaendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya kutenda makosa hayo ya udhalilishaji katika jamii.