Zenj FM
Zenj FM
21 June 2026, 20:19

Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Kati, Dkt. Mwanaisha Ali Said, amewataka wananchi kuendelea kudumisha usafi wa mazingira kwa kuwa ni jukumu la kila mmoja katika jamii. Akikabidhi madasbini katika Kituo cha Watoto Yatima cha Maftuh Foundation, Kibele, amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha watoto wanaishi katika mazingira safi na salama dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na uchafu.
Na Hakika Mwinyi.
Wananchi wametakiwa kuendelea kudumisha usafi na kutunza mazingira katika maeneo yanayowazunguka, kwa kuwa jukumu hilo ni la kila mmoja na si la Manispaa pekee.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Kati, Dkt. Mwanaisha Ali Said, wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya kuhifadhia taka (madasbini) katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Maftuh Foundation kilichopo Kibele, Wilaya ya Kati Unguja.
Dkt. Mwanaisha amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha usafi wa mazingira katika kituo hicho ili kuhakikisha watoto wanaishi katika mazingira salama na yenye afya, pamoja na kujikinga dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na uchafu.
Aidha, amesisitiza kuwa usafi wa mazingira ni msingi muhimu wa afya bora na maendeleo ya jamii, hivyo wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi mazingira yao.
Kwa upande wake, Katibu wa Maftuh Foundation, Hamad Juma Abdallah, ameishukuru Manispaa Kati kwa msaada huo akieleza kuwa madasbini hayo yatasaidia katika uhifadhi sahihi wa taka zinazozalishwa katika kituo hicho.
Amesema uongozi wa kituo hicho umejipanga kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kutumika ipasavyo ili kufanikisha azma ya kuwa na mazingira safi na salama kwa watoto wanaolelewa hapo.
Kituo cha Maftuh Foundation kinahudumia jumla ya watoto 52, ambapo watoto wa kiume ni 22 na watoto wa kike ni 30.