Zenj FM

Zanzibar yaimarisha malezi ya awali kwa kujenga vituo vya kulelea watoto

22 July 2026, 17:30

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto Zanzibar sambamba na ufunguzi wa Kituo cha kulelea watoto katika Soko la Mwanakwerekwe.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imezindua Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto pamoja na Kituo cha Kulelea Watoto katika Soko la Mwanakwerekwe, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ustawi wa mtoto na kuwawezesha akina mama kufanya shughuli za kiuchumi kwa utulivu. Serikali imesema mpango huo unalenga kujenga kizazi chenye afya, elimu na maadili bora kupitia uwekezaji katika malezi ya watoto tangu wakiwa wadogo.

Na Mary Julius.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amesema uwekezaji katika malezi na makuzi ya mtoto wa umri wa awali ni msingi wa kujenga kizazi chenye wataalamu na viongozi wazuri wa baadaye.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla  ameyasema hayo kwa niaba ya  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dkt.  Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya uzinduzi wa Programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto Zanzibar sambamba na ufunguzi wa Kituo cha kulelea watoto katika Soko la Mwanakwerekwe.

Amesema kituo hicho kinatekeleza maono ya Rais wa Zanzibar ya kuhakikisha watoto wanapata malezi bora tangu wakiwa wadogo, huku akiwataka wazazi kufuata ushauri wa wataalamu katika malezi ya watoto.

Aidha ameipongeza Stanbic Bank, na Save the Children kwa kuunga mkono juhudi za Serikali, huku akizihimiza taasisi nyingine kuiga mfano huo.

Sauti ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla.

Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Anna Atanas Poul amesema kituo hicho kitawapunguzia mzigo akina mama wafanyabiashara kwa kutoa huduma za malezi, lishe na sehemu ya kunyonyesha.

Aidha amesema mpango wa Serikali ni kujenga vituo kama hivyo katika masoko mengine Zanzibar na ofisi za umma.

Sauti ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Anna Atanas Poul.

Naye Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Stanbic Tanzania, Derrick Lugemalila, amesema nchi nyingi bado hawajalipa kipaombele suala la makuzi ya awali ya mtoto hivyo kupitia programu hio watahakikisha watoto wote wa Zanzibar wananufaika na kushiriki kikamilifu katika program hiyo itakayowakuza na kuwapatia ulinzi.

Sauti ya Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Stanbic Tanzania, Derrick Lugemalila.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Huduma za Jamii, Ofisi ya Rais Ikulu, Dk. Ibrahimu Kabole, amesema kituo hicho ni sehemu ya mradi mkubwa wa maendeleo ya mtoto Zanzibar unaolenga kuwaondoa watoto katika mazingira hatarishi ya masokoni, huku akibainisha kuwa vituo vinane vitajengwa kwa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi.

Sauti ya Msimamizi wa Huduma za Jamii, Ofisi ya Rais Ikulu, Dk. Ibrahimu Kabole.

Naye Afisa wa Save the Children, Angela Kayalem, amesema mradi huo unaunga mkono malengo ya Serikali ya kuimarisha malezi ya watoto, akieleza kuwa kituo hicho kitahudumia watoto 60 na kusaidia akina mama kufanya biashara kwa utulivu huku watoto wao wakiwa salama.

Sauti ya Afisa wa Save the Children, Angela Kayalem.

Wakizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa Soko la Mwanakwerekwe, wameishukuru Serikali na wadau kwa ujenzi wa kituo hicho, wakisema kitawapunguzia changamoto ya kuwalea watoto wakati wa biashara na kuongeza fursa ya kukuza kipato chao.

Wafanya biashara.