Zenj FM
Zenj FM
12 August 2026, 20:39

Sukhayla Omar Hamad alifanikiwa kuwa Diwani wa Wadi ya Mtambwe licha ya kukutana na maneno ya kukatisha tamaa, akiamini katika Mungu, uwezo wake na juhudi zake. Safari yake ni mfano kwa wanawake na vijana kwamba wanapaswa kujiamini, kutumia fursa za uongozi na kutokubali vikwazo viwakatishe tamaa.
Na Is-Haka Mohamed – Pemba
Kuna hadithi ya zamani ya fasihi simulizi inayosimulia kuhusu kundi la vyura waliotakiwa kupanda mnazi mrefu. Wakati baadhi yao walipoanza kupanda, vyura waliokuwa chini walianza kuwapigia kelele na kuwakatisha tamaa.
“Wewe utaanguka! Shuka! Huwezi! Kuna miiba! Kuna viwembe! Kuna misumari!”
Kwa kusikia kelele hizo, baadhi ya vyura waliokuwa wameanza kupanda walirudi nyuma taratibu hadi chini. Lakini mmoja wao aliendelea kupanda bila kujali kelele zilizokuwa zikisikika kutoka chini. Alifanikiwa kufika kileleni mwa mnazi na kupata alichokuwa anakitafuta.
Baadaye iligundulika kuwa chura huyo alikuwa kiziwi. Hakuwa akisikia maneno ya waliokuwa wakimkatisha tamaa.
Ni hadithi hii ambayo kwa namna fulani inaakisi safari ya uongozi ya Sukhayla Omar Hamad, Diwani wa Wadi ya Mtambwe, ambaye anasema alilazimika “kuziba masikio” yake dhidi ya maneno ya watu waliokuwa wakimkatisha tamaa katika hatua zake za kisiasa.
Sukhayla anasema, wakati alipoamua kuingia katika siasa na kuwania nafasi ya udiwani, baadhi ya watu walimwambia kuwa elimu yake ingewafanya wengine kukosa nafasi, huku wengine wakimshauri aachane na siasa za upinzani kwa madai kuwa angeweza “kuharibu CV yake”.
“Wapo waliokuwa wakisema kijana huyu kasoma, usomi wake utatufanya sisi wengine tusipate nafasi, bora asipewe hii nafasi. Wengine walikuwa wakiniambia niache siasa za upinzani kwa sababu mimi ni msomi nisije nikajiharibia,” anasema Sukhayla.
Mbali na maneno hayo, anasema kulikuwa na watu waliokuwa wakimwambia waziwazi na hata kumuombea asipewe nafasi ya uongozi.
Lakini badala ya kurudi nyuma, Sukhayla aliamua kujiamini.
“Niliweka imani kwamba mkinipa mimi nitakuwa kiongozi, msiponipa nimeshaongeza CV yangu. Nikiamini jitihada ina Mungu. Mimi ni kijana shupavu, nimejiamini na nimejitoa kwa hali na mali kutetea taifa na watu wote kwa ujumla,” anasema.
Alipata Wapi Ujasiri wa Kugombea Udiwani?
Kwa Sukhayla, uamuzi wa kuwania udiwani haukuwa wa mtu mmoja. Anaeleza kuwa familia yake pamoja na viongozi wa chama katika ngazi ya wadi, jimbo na mkoa waliona uwezo aliokuwa nao na kumuunga mkono.
Hata hivyo, baadhi ya wanachama na watu waliokuwa karibu naye walimrudisha nyuma kwa maneno ya kukatisha tamaa.
“Familia yangu, viongozi wangu wa chama wadi, jimbo na mkoa waliona naweza na wakaniunga mkono. Jamii na baadhi ya wanachama wenzangu ndio walikuwa wakinirudisha nyuma kwa maneno, lakini sikutishika. Niliomba Mungu na huko ndiko kulikonipa ujasiri,” anaeleza.
Anaamini kuwa kumtanguliza Mungu katika kila jambo kulimsaidia kuvuka hofu.
“Kila jambo ukimtanguliza Mungu mbele, hakuna ugumu,” anasema.
Sukhayla alijaribu kwa mara ya kwanza na kufanikiwa. Leo anaendelea na harakati za kuisaidia jamii, hususan vijana na wanawake katika Wadi ya Mtambwe.
Anasema jambo lililomsukuma zaidi ni swali alilokuwa akijiuliza kuhusu uwezo wa vijana, hasa wanawake, kushiriki katika uongozi.
“Nilijiuliza, kwa nini vijana tusiweze, na hususan sisi wanawake, kwa nini tukatishwe tamaa? Nikapata ujasiri kwamba naweza bila kujali maneno. Nikajitosa kuchukua fomu. Ilikuwa mara yangu ya kwanza, lakini nilifanikiwa bila kupingwa,” anasema.
Watu Wa Karibu Wanasemaje?
Mpaji Abass, mwanachama wa ACT Wazalendo anayemfahamu Sukhayla kupitia harakati za chama, anaamini bado ana nafasi kubwa ya kupanda zaidi katika uongozi.
Anasema endapo Sukhayla ataendelea na ujasiri, uwezo na uthubutu alionao sasa kama Diwani wa Mtambwe, anaweza kufikia nafasi kubwa zaidi za uongozi kutokana na uwezo wake.
Kwa upande wake, Maryam Nuhu, mwanamke anayemfuatilia Sukhayla katika safari yake ya uongozi, anamwona kama mfano wa kuigwa na wanawake vijana wanaotamani kuingia katika siasa.
“Ninajifunza mengi kupitia viongozi wanawake.
Diwani Sukhayla ninakutana naye katika masuala ya chama. Maono yake na namna anavyotutia moyo sisi ambao uongozi bado ni nia tu, tunapata ujasiri mkubwa wa kutimiza ndoto zetu,” anasema Maryam.
Anaongeza kuwa namna Sukhayla anavyopambana na kufanya utetezi katika kukabiliana na vikwazo imempa matumaini kuwa siasa si lazima ziwe za chama tawala pekee.
Wito Kwa Wanawake
Sukhayla anawataka wanawake wenzake kutokuogopa vikwazo wanapopata fursa za kushiriki katika uongozi.
Kwa mtazamo wake, mafanikio katika siasa yanahitaji ujasiri, uthubutu na uwezo wa kukabiliana na maneno ya kukatisha tamaa.
“Mtu yeyote anapoona fursa asiogope kuifikia na kuonesha alicho nacho katika kuitumia fursa. Wala tusijenge imani kwamba ukiwa mpinzani unaharibu CV yako. Bidii haimtupi mtu, hata akiwa katika chama gani,” anasema.
Tamwa Zanzibar: Wanawake Wasiache Fursa
Katika makala hii, TAMWA Zanzibar pia inasisitiza umuhimu wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuzichangamkia fursa za uongozi.
Mratibu wa TAMWA Zanzibar, Amina Ahmed, anasema ushiriki wa makundi hayo katika vyombo vya maamuzi ni muhimu katika kuongeza idadi ya wanawake na kufikia lengo la uwakilishi wa 50 kwa 50.
Wanawake Kutoka Vyama Tofauti Wamjua Sukhayla
Licha ya kuwa katika vyama vyenye mrengo tofauti, Indra Mohammed, Diwani wa CCM wa Wadi ya Konde, anasema amemfahamu Sukhayla kwa karibu tangu walipoanza kukutana katika harakati za uongozi.
Anamuelezea kama mwanamke mwenye ujasiri na anayesimamia mambo anayoyaamini, hususan katika masuala ya maendeleo.
Mtumwa Said Muhammed naye anasema Sukhayla ni mwanamke asiyeogopa anapodhamiria kukitetea chama chake na wananchi, jambo analoliona kuwa ni sehemu ya ujasiri wake.
Safari ya Sukhayla Omar Hamad kwa hiyo haijaishia kwenye kushinda nafasi ya udiwani. Ni simulizi ya kijana aliyekutana na maneno ya kukatisha tamaa, lakini akaamua kuyachukulia kama kelele za mbali.
Kama yule “chura kiziwi”, aliziba masikio, akatazama kilele na kuendelea kupanda.
Na kwa Sukhayla, kilele hicho kinaweza kuwa mwanzo tu wa safari ndefu zaidi katika uongozi.