Zenj FM

Zanzibar yaweka vituo 17 kuzikabili athari za el niño

23 September 2026, 22:06

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Mgereza Miraji Mzee, akizungumaza katika mkutano wa uratibu wa maandalizi ya kukabiliana na mvua hizo, uliohusisha makatibu wakuu na taasisi mbalimbali za uokozi.Picha na Wizara ya Afya Zanzibar.

Wizara ya Afya Zanzibar imejiandaa kukabiliana na athari za mvua kubwa za El Niño kwa kutenga vituo 17 vya afya na zaidi ya magari 20 ya wagonjwa kwa huduma za dharura. Serikali pia imewaandaa watumishi wa afya na kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa.

Na Mary Julius.

Wizara ya Afya Zanzibar imetenga vituo vya afya na zahanati 17 Unguja na Pemba kwa ajili ya kutoa huduma za dharura endapo mvua kubwa zinazoambatana na El Niño zitasababisha athari kwa wananchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Mgereza Miraji Mzee, ameyasema hayo katika mkutano wa uratibu wa maandalizi ya kukabiliana na mvua hizo, uliohusisha makatibu wakuu na taasisi mbalimbali za uokozi,amesema vituo 12 vipo Unguja na vitano Pemba, huku zaidi ya magari 20 ya wagonjwa, Ambulance, yakitengwa kwa ajili ya dharura hizo.

Amesema Bohari Kuu ya Dawa ina akiba ya kutosha ya dawa za dharura na dawa za kawaida, huku dawa, vifaa tiba, vifaa vya kinga na watumishi wa afya vikiwa vimeandaliwa.

Dk. Mgereza amesema watumishi 168 wa afya wamepatiwa mafunzo ya kukabiliana na dharura, huku zaidi ya wahudumu 2,300 wa afya ngazi ya jamii wakitumiwa kufuatilia hali katika shehia na kutoa taarifa za matukio hatarishi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Katiba na Sheria, Mzee Ali Haji, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kukabiliana na athari za mvua kupitia ushirikiano wa taasisi mbalimbali za uokozi, afya na tahadhari za mapema.

Amewataka wananchi wa maeneo ya mabondeni, nyumba zisizo imara na maeneo yanayotuamisha maji kuchukua tahadhari na kuhama wanapoelekezwa na mamlaka.

Sauti ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Katiba na Sheria, Mzee Ali Haji.

Naye Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya, Dk. Faiza Bwanaheri Abass, amesema tathmini imebaini shehia 42 ziko katika hatari ya kukumbwa na magonjwa ya kuharisha, zikiwemo 36 Unguja na sita Pemba.

Amesema pia shehia 25 za Unguja ziko katika hatari ya kuongezeka kwa malaria kutokana na maji kutuama wakati wa mvua.

Dk. Faiza amesema Wizara imeimarisha mfumo wa kutoa taarifa za milipuko ya magonjwa, maandalizi ya dawa za kutibu maji na elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya maji salama.

Sauti ya Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya, Dk. Faiza Bwanaheri Abass,akielezea zaidi

Nao Wadau walioshiriki mkutano huo wameipongeza Wizara ya Afya kwa maandalizi hayo na kuahidi kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa.