Zenj FM

Skuli ya Kiponda kuwa skuli ya utalii, serikali yatoa kauli

10 October 2026, 22:51

Naibu Katibu Mkuu wa Taaluma, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Amosi John Henock,akizungumza katika Mahafali ya 21 ya Skuli ya Sekondari Kiponda yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Afya Shaa.

Serikali ya Zanzibar ya Mapinduzi ya Zanzibar yaweka mikakati mipya ya kuimarisha elimu, huku Skuli ya Kiponda ikitarajiwa kuwa maalumu kwa masomo ya utalii.

Na Mary Julius.

Naibu Katibu Mkuu wa Taaluma, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Amosi John Henock, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  inaendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu ya skuli, maslahi ya walimu na mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Akizungumza katika Mahafali ya 21 ya Skuli ya Sekondari Kiponda yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Afya Shaa Mchina, Mwanzo, Wilaya ya Magharibi B, Henock amesema Serikali imeajiri walimu wapya 1,500 na inaendelea na mipango ya kuboresha maslahi yao.

Amesema Wizara pia inaandaa mpango wa kuifanya Skuli ya Sekondari Kiponda kuwa skuli maalumu inayolenga masomo ya utalii, sambamba na kuimarisha ufundishaji wa lugha mbalimbali ili kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira.

Aidha, amewapongeza wahitimu wa kidato cha sita kwa kufikia hatua hiyo muhimu ya elimu yao, huku akiwataka wazazi kuendelea kushirikiana na walimu katika kuwawezesha watoto wao kutimiza ndoto zao.

Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Kiponda, Miza Kai Khamisi.

Naye Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Kiponda, Miza Kai Khamisi, amewataka wahitimu kuzingatia tabia njema, nidhamu binafsi na uwajibikaji, akisisitiza kuwa taifa linawategemea katika maendeleo ya baadaye.

Sauti ya Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Kiponda, Miza Kai Khamisi.

Akisoma   risala ya wahitimu, Seleimani Othuman ameitaja changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyoathiri ratiba ya masomo, hali inayosababisha wanafunzi kusoma masomo nane badala ya masomo kumi kwa siku.

Sauti ya Risala ya wahitimu, Seleimani Othuman.