Zenj FM

Zanzibar kuandika historia! Mameneja wa rasilimali watu Afrika kukutana

7 November 2026, 14:30

Rais wa Mtandao wa Mameneja wa Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika (APS HRMnet), Xavier Daud, akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa wizara Mazizini,

Rais wa APS HRMnet, Xavier Daud, amesema maandalizi ya Mkutano wa 11 wa Mameneja wa Rasilimali Watu wa Utumishi wa Umma Barani Afrika,utakaofanyika Zanzibar kuanzia Novemba 10 hadi 13, 2026, umefikia asilimia 90 huku washiriki wapatao 1,200 wakitarajiwa kuhudhuria. Mkutano huo utajadili matumizi ya akili bandia katika kuboresha usimamizi wa rasilimali watu na kuimarisha utendaji wa sekta ya umma barani Afrika.

Na Mary Julius.

Rais wa Mtandao wa Mameneja wa Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika (APS HRMnet), Xavier Daud, amesema maandalizi ya Mkutano wa 11 wa mtandao huo yamefikia zaidi ya asilimia 90, huku washiriki wapatao 1,200 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wakithibitisha kushiriki.

Akizungumza na waandishi wa habari Zanzibar, Xavier amesema mkutano huo utafanyika Novemba 10 hadi 13, 2026, katika Hoteli ya Verde Zanzibar, baada ya kuhamishwa kutoka Hoteli ya Golden Tulip kutokana na ongezeko la washiriki.

Amesema mkutano huo utajadili matumizi ya akili bandia katika kuboresha usimamizi wa rasilimali watu na kuongeza ufanisi wa utumishi wa umma barani Afrika.

Aidha Xavier amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Husien Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa  mgeni rasmi, huku usajili wa washiriki wa ndani ukifanyika Novemba 8 na washiriki kutoka nje ya nchi Novemba 9, katika Hoteli ya Verde Zanzibar.

Sauti ya Rais wa Mtandao wa Mameneja wa Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika (APS HRMnet), Xavier Daud.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa APS HRMnet anayewakilisha Afrika Mashariki Florence Wanguku amesema mkutano huo utatoa fursa kwa mameneja wa rasilimali watu kubadilishana ujuzi na uzoefu kuhusu matumizi ya akili bandia katika kuboresha mifumo ya utendaji wa taasisi za umma.

,Sauti ya Makamu wa Rais wa APS HRMnet anayewakilisha Afrika Mashariki Florence Wanguku.

Mkutano huo wa siku nne unatarajiwa kuwa jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa Afrika katika matumizi ya teknolojia na mageuzi ya usimamizi wa rasilimali watu katika utumishi wa umma.