Zenj FM
Zenj FM
26 October 2026, 15:20

ZAPONET Zanzibar yaweka mikakati mipya ya kuimarisha uwajibikaji, kuboresha uongozi na kujenga taasisi imara isiyotegemea wafadhili pekee. Je, mapitio ya katiba na nyaraka zake yatafungua ukurasa mpya kwa jumuiya za wasaidizi wa sheria Zanzibar katika kutoa huduma bora kwa wananchi?
Na Mary Julius.
Taasisi ya Mwamvuli wa Wasaidizi wa Sheria Zanzibar, ZAPONET, imeanza kufanya mapitio ya katiba na nyaraka zake muhimu kwa lengo la kuimarisha mifumo ya uendeshaji, kuongeza uwajibikaji na kujenga uwezo wa kujitegemea kwa kutumia rasilimali za ndani badala ya kutegemea wafadhili pekee.
Hatua hiyo inalenga kuifanya taasisi hiyo kuwa imara, yenye ufanisi na inayoweza kuendeleza shughuli zake kwa manufaa ya wanachama wake.
Akizungumza katika kikao cha mapitio hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa ZAPONET, Asia A. Hussein, amesema kupitia upya katiba na nyaraka za taasisi hiyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha zinaendana na mahitaji ya sasa na kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake.
Aidha amesema mapitio hayo yatasaidia kuweka mifumo bora ya kiutendaji na kuhakikisha taasisi inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mshauri Elekezi ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya IMED Dkt. Dorath Olomi, amesema taasisi zinapaswa kujenga mifumo imara itakayozisaidia kujiendesha kwa kutumia rasilimali zilizopo, na kusisitiza umuhimu wa kuwa na taswira nzuri inayojenga imani kwa wadau na Serikali.
Amesema kikao hicho pia kinalenga kujadili njia mbalimbali za kuimarisha ZAPONET, ikiwemo kuweka mgawanyo mzuri wa majukumu kati ya bodi na watendaji, ili kila upande uweze kutekeleza wajibu wake bila kuingiliana na kuongeza ufanisi wa taasisi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ZAPONET, Nassor Hakim Haji, amesema kikao hicho kitasaidia kuimarisha taasisi hiyo kama mwamvuli wa jumuiya za wasaidizi wa sheria Zanzibar na kuweka misingi itakayoiwezesha kujitegemea na kuendelea kutoa manufaa kwa wanachama wake.
Amewasisitiza viongozi kuhakikisha mapendekezo yaliyotolewa katika kikao hicho yanafikishwa kwa wadau kwa ajili ya kutoa maoni, ili kupatikana kwa katiba inayokidhi mahitaji ya taasisi na kuimarisha utendaji wake.
Kwa upande wake, mjumbe kutoka Pemba ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Micheweni, Saleh Hamad Juma, amesema mafunzo na majadiliano hayo yatawasaidia viongozi kuimarisha jumuiya wanazoziongoza kwa kuweka wazi majukumu ya kila kiongozi na mtendaji.
Amesema utaratibu huo utasaidia kuondoa mwingiliano wa majukumu, kuongeza uwajibikaji na kuwezesha jumuiya kufanya kazi kwa ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi.
Kikao hicho kimefadhiliwa na Enabel chini ya mwamvuli wa ZAPONET, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuzijengea uwezo jumuiya za wasaidizi wa sheria Zanzibar ili ziweze kuimarisha mifumo yao ya uendeshaji na kujitegemea katika utekelezaji wa majukumu yao.