Zenj FM

Wananchi 62% wamesajiliwa ZHSF, sekta isiyo rasmi yaibua changamoto

1 October 2026, 23:21

Mtafiti Mwandamizi wa Afya, Dk. Fatuma Manzi, akikiwa katika kikao cha uwasilishaji wa matokeo ya awamu ya kwanza ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar kwa kushirikiana na PharmAccess.

Utafiti wa awali umeonyesha kuwa asilimia 62 ya wananchi wa Zanzibar tayari wamesajiliwa katika Mfuko wa bima ya Afya Zanzibar. Watafiti wamependekeza hatua zaidi za kuhakikisha wanachama wanaendelea kuchangia na kupata huduma bora za afya.

Na Mary Julius.

Mtafiti Mwandamizi wa Afya, Dk. Fatuma Manzi, amesema asilimia 62 ya wananchi wa Zanzibar tayari wamejiandikisha katika Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar.

Dk. Fatuma amesema kuna umuhimu wa kufanya tathmini ya ndani mara kwa mara ili kuhakikisha wanachama wanaendelea kuchangia kila mwaka na hivyo kuufanya mfuko huo kuwa endelevu.

Amesema hayo wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya awamu ya kwanza ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar kwa kushirikiana na PharmAccess, kwa lengo la kubaini mafanikio na changamoto zilizojitokeza tangu kuanzishwa kwa mfuko huo.

Dk. Fatuma amesema miongoni mwa changamoto kubwa ni namna ya kuwawezesha wananchi wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi kuendelea kuchangia mfuko huo.

Aidha Dk Fatuma amesema kuna umuhimu wa kuboresha mifumo ya usajili ili kutambua kwa usahihi wananchi wanaostahili kusaidiwa na Serikali.

Sauti ya Mtafiti Mwandamizi wa Afya, Dk. Fatuma Manzi,

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti wa Wizara ya Afya Zanzibar, Omar Mwalimu, amesema tathmini hiyo haina lengo la kuangalia mapungufu pekee, bali kubaini changamoto na kuzifanyia kazi ili wananchi wengi zaidi wanufaike na mfuko huo.

Omar amesema matokeo ya utafiti huo yatasaidia kuboresha mfumo na kuweka sera rafiki zitakazowawezesha wananchi kuendelea kuchangia na kupata huduma bora za afya.

Sauti ya Mkurugenzi wa Mipango, Sera na Utafiti wa Wizara ya Afya Zanzibar, Omar Mwalimu.

Naye Msimamizi Mkuu wa Utafiti kutoka PharmAccess, Ramadhani Abdul, ameishukuru Wizara ya Afya kwa ushirikiano uliotolewa katika utafiti huo.

Amesema utafiti wa awali umeibua maoni na mapendekezo ambayo yatasaidia kuufanya Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar kuwa imara na endelevu.

Sauti ya Msimamizi Mkuu wa Utafiti kutoka PharmAccess, Ramadhani Abdul.