Zenj FM

Kustaafu bila wasiwasi, vijana waaswa kuwekeza

8 November 2026, 21:19

Mohammed Hija Mashaka akiwana Kayagamba katika hafla ya kumuaga Mohammed.

Mratibu wa Programu na Mafunzo kutoka Chama Kikuu cha Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Tanzania, Leah Daudi Mbilinyi, amewataka vijana kuanza kuweka akiba na kuwekeza mapema wanapoanza kupata ajira. Wito huo umetolewa katika hafla ya kumuaga mstaafu wa TRA Zanzibar, Mohammed Hija Mashaka, aliyehimiza wafanyakazi kujiunga na SACCOS ili kujiandaa na maisha baada ya ajira.

Na Mary Julis.

Mratibu wa Programu na Mafunzo kutoka Chama Kikuu cha Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Tanzania, Leah Daudi Mbilinyi, amewataka vijana kuanza kuweka akiba na kuwekeza mara wanapoanza kupata ajira na kipato, ili kujiandaa na maisha baada ya kustaafu na kuepuka kuwa mzigo kwa jamii.

Leah ameyasema hayo katika hafla ya kumuaga mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar, Mohammed Hija Mashaka, anayestaafu utumishi wa umma, akisisitiza kuwa hakuna uwekezaji mdogo kwani hata kiasi kidogo kinaweza kuwa msingi wa maisha bora ya baadaye.

Amesema Mohammed amekuwa mfano wa kuigwa kupitia nafasi yake ya uenyekiti wa TRA SACCOS LTD Tawi la Zanzibar, ambapo ameweza kuwahamasisha vijana wengi kujiunga na chama hicho ili waweze kunufaika na utaratibu wa kuweka akiba na kukopa.

Ameeleza kuwa kwa sasa SACCOS zenye leseni nchini zimefikia 900, zikiwa na wanachama wapatao milioni 1.2, huku asilimia 58 zikiwa ni SACCOS za wafanyakazi.

Sauti ya Mratibu wa Programu na Mafunzo kutoka Chama Kikuu cha Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo Tanzania, Leah Daudi Mbilinyi.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kazi Maalum wa TRA Zanzibar, Saleh Haji Pandu, amemtaka Mohammed kuendelea kuwa jicho la TRA hata baada ya kustaafu, kwa kutoa ushauri na taarifa pale anapoona changamoto zinazoweza kuathiri taswira ya taasisi hiyo ili ziweze kufanyiwa marekebisho.

Naye Meneja wa Forodha Zanzibar, Suleiman Saidi, amemshukuru Mohammed kwa ushirikiano aliouonesha wakati wa utumishi wake, akisema amekuwa zaidi ya mfanyakazi mwenzake bali ndugu na rafiki.

Aidha  Amemuomba kuacha milango wazi ili watendaji wa TRA waendelee kunufaika na hekima na busara zake.

Kwa upande wake, mstaafu Mohammed Hija Mashaka amewataka wafanyakazi wanaoendelea na utumishi kuhakikisha wanaweka akiba, wanafanya kazi kwa uadilifu na nidhamu, pamoja na kutunza afya zao ili kujiandaa na maisha ya baada ya ajira.

Aidha, amewahimiza wafanyakazi kujiunga na SACCOS akieleza kuwa ushirika huo unatoa fursa ya kuweka akiba na kupata mikopo, huku ukiwajengea wanachama utamaduni wa kupanga na kujiandaa kifedha kwa maisha ya baadaye.

Sauti ya Mohammed Hija Mashaka.