Zenj FM
Zenj FM
2 November 2026, 11:13

Hafla ya kuwaaga walimu wastaafu wa Skuli ya Hamamni Zanzibar imeibua ujumbe mzito kuhusu uzalendo na nidhamu kazini, huku Mkurugenzi wa Idara ya Michezo na Utamaduni, Hafsa Aboud Talibu, akiwataka watumishi wa sasa kuiga mfano wa walimu wa zamani waliojitolea kwa moyo katika kazi ya ualimu.
Zulfa Ameir.
Mkurugenzi wa Idara ya Michezo na Utamaduni, Hafsa Aboud Talibu, amempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuweka utaratibu wa utoaji wa posho kwa walimu.
Hafsa ameyasema hayo katika hafla fupi ya kuwaaga walimu wastaafu iliyofanyika katika Shule ya Hamamni, iliyopo Mji Mkongwe Zanzibar, ambapo pia amewapongeza walimu hao kwa utumishi wao uliotukuka.
Hafsa amesema utaratibu huo ni jambo la kutia moyo kwa watumishi, kazi ya ualimu inahitaji uzalendo, moyo wa kujitolea na uvumilivu.
Amesema walimu hao wamefikia hatua ya kustaafu wakiwa wameonesha uzalendo na kujitolea kwa muda mrefu, tofauti na baadhi ya watumishi wa sasa ambao, kwa maelezo yake, wanapoingia kazini huanza kuulizia maslahi na posho kabla ya kuzingatia majukumu yao.
Aidha, amewataka watumishi wanaoingia katika utumishi wa umma kuzingatia mikataba yao, kutekeleza majukumu kwa mujibu wa nafasi zao na kuwa na nidhamu ya kazi bila kusubiri kufuatiliwa kila mara.
Katika hatua nyingine, amewataka walimu kutoa fursa kwa wanafunzi kushiriki kikamilifu katika michezo mbalimbali, akieleza kuwa michezo ina mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya akili, kujenga nidhamu na kupunguza vitendo vya unyanyasaji miongoni mwa wanafunzi.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Hamamni, Khamis Hamad Khamis, ametoa pongezi kwa walimu wastaafu, Asia Iddi Ali na Fatma Makame Pando, kwa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya shule hiyo.
Amesema walimu hao wamekuwa nguzo muhimu katika mafanikio ya shule kutokana na uchapakazi, uaminifu na moyo wa kujitolea waliouonesha katika kipindi chote walichohudumu, huku akiwataka walimu wengine kuiga mfano wao katika kutekeleza majukumu yao.
Nao walimu wastaafu, Asia Iddi Ali na Fatma Makame Pando, wamesema licha ya kuhitimisha utumishi wao rasmi, bado wataendelea kuwa sehemu ya familia ya Skuli ya Hamamni na kudumisha uhusiano mwema na wenzao.