Zenj FM
Zenj FM
2 November 2026, 20:07

Wakandarasi waliokabidhiwa mradi wa kujenga Vizimba vya kuhifadhia taka wametakiwa kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa kama walivyokubaliana katika mkataba.
Hayo ameyasema Msatahiki Meya wa Baraza la Manispaa Kati Said Hassan Shaaban wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo huko Wilaya ya Kati.
Amesema mradi huo umefikia asilimia 20 jambo ambalo ni kinyume na makubaliano ya makataba walioandikiana ambapo ndani ya miezi tisa mradi huo uwe umekamilika kwa asilimia 100.
Kwa upande wake Injinia kutoka Kampuni ya Faster Limited Joji Moris ameiomba Serikali kupitia Baraza la Manispaa Kati kuwaongezea muda wa mkataba wa ujenzi wa Vizimba hivyo ili kuweza kukabidhi mradi huo kwa wananchi ukiwa tayari umekamilika.
Nae Sheha wa Shehia ya Jumbi Muhidini Haji Machano amewataka wananchi wa Shehia hiyo na Shehia jirani kueka taka maeneo rasmin yaliyotengewa na Serikali ili kuepukana na kuzagaa taka mitaani.
Sambamba na hayo nae Kikombe Jaku Haji mwananchi wa Shehia ya Jumbi kwa niaba ya wananchi wenzake amesema, wamefarijika sana kuona Serikali inawajengea Vizimba vya kuhifadhia taka katika maeneo yao, kwani hawana sehemu rasmi ya kutupa taka kulingana na ukuaji wa mji pia kuiomba Serikali ujenzi uwe wa haraka ili kuepuka kutupa taka ovyo katika maeneo wanayoishi.
Jumla ya vizimba kumi vinatarijwa kujengwa ndani ya wilaya Kati na ziara hiyo imejumuisha shehia ya Jumbi, Tunguu pamoja na Binguni yenye lengo la kukagua mradi wa vizimba vya kuhifadhia taka.