Zenj FM
Zenj FM
9 October 2026, 17:41

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zubeir Ali Maulid, amesisitiza kuwa msaada wa kisheria ni haki ya kila mwananchi, huku akihimiza kuimarishwa kwa huduma hizo ili wananchi waweze kupata haki bila vikwazo
Na Mary Julius.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zubeir Ali Maulid, amesema huduma za msaada wa kisheria zina nafasi muhimu katika kuhakikisha wananchi wanafahamu haki zao, wanapata ushauri wa kisheria na wanapata fursa ya kutendewa haki bila vikwazo vya elimu, uwezo wa kifedha au umbali wa kijiografia.
Akizungumza katika kilele cha Wiki ya Msaada wa Kisheria, Maisara, amesema bado juhudi zinahitajika ili kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao na namna ya kuzidai kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohammed Ali Abdalla, amesema wananchi 367 wamefikiwa na huduma hizo, migogoro 95 imetatuliwa, sawa na asilimia 26, huku mingine 272 ikiendelea kushughulikiwa.
Amehimiza wasaidizi wa kisheria kutoa elimu mashuleni kuhusu matumizi ya simu na athari zake za kijamii na kiuchumi, pamoja na kushirikiana na masheha 121 wa mkoa huo kuwafikishia wananchi elimu ya sheria kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Enabel, Christina Mdemu, ameishukuru Serikali kwa ushirikiano katika kuboresha mradi wa Sauti ya Wanawake na kuimarisha huduma za kisheria kupitia mifumo ya kidijitali.
Naye Mwakilishi wa watoa huduma za msaada wa kisheria, Shaabani Sariboko Makarani, amesema licha ya mafunzo, vifaa vya kidijitali na bajaji saba walizopatiwa kusaidia kuwafikia wananchi, bado wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa ofisi na gharama za kufuatilia kesi. Ameomba Serikali kuwapatia ofisi na kuweka utaratibu wa posho za usafiri.
Maadhimisho hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu “Msaada wa Kisheria: Mwananchi Ijue Haki, Upate Haki,” huku Spika Zubeir Ali Maulid akikabidhi tuzo kwa wadau waliofanya vizuri katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria.