Zenj FM
Zenj FM
13 November 2026, 15:39

Serikali ya Zanzibar yapunguza faini za makosa ya bodaboda na bajaji, huku ikitangaza viwango vipya vya mwendo barabarani vitakavyoanza kutumika Desemba Mosi, 2026. Je, ni faini zipi zimepunguzwa na mwendo unaoruhusiwa ni upi? Tazama taarifa hii kufahamu mabadiliko yote yaliyotangazwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Khalid Salum Mohamed.
Na Mary Julius.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohamed, ametangaza marekebisho ya viwango vya faini kwa makosa mbalimbali ya usafiri wa pikipiki na bajaji, hatua inayolenga kuzingatia maoni ya madereva na kuboresha mazingira ya usafiri bila kuathiri usalama barabarani.
Akitoa taarifa hiyo, kwa waandishi wa habari Waziri Dkt. Khalid amesema Serikali imepunguza faini ya kuendesha chombo bila usajili kutoka shilingi 699,000 hadi 100,000, bila leseni ya njia kutoka 466,000 hadi 50,000, huku faini ya kutovaa kofia ngumu (Helmet) ikishuka kutoka shilingi 80,000 hadi 30,000.
Amesema marekebisho mengine ni faini ya kuendesha bila leseni ya udereva kutoka shilingi 116,000 hadi 50,000, kutoa huduma bila leseni ya biashara kutoka 100,000 hadi 50,000, pamoja na kuendesha kwa mwendo mkubwa kutoka shilingi 233,000 hadi 50,000.
Katika hatua nyingine,waziri aamesema Serikali imeweka viwango vipya vya mwendo, ambapo maeneo ya biashara, skuli, hospitali, Mji Mkongwe na maeneo yenye mikusanyiko ya watu yatakuwa na kiwango cha juu cha kilomita 30 kwa saa, huku wakati wa mvua magari yote yakitakiwa kutotumia mwendo unaozidi kilomita 30 kwa saa.
Ameeleza kuwa viwango vya mwendo katika barabara za ndani vitakuwa kilomita 60 kwa saa, huku barabara kuu ndani ya miji na zinazoingia mijini zikiruhusiwa kufikia kilomita 80 kwa saa, isipokuwa pale alama za barabarani zitakapoelekeza vinginevyo.
Aidha Dkt. Khalid amesema marekebisho hayo yataanza kutekelezwa rasmi Desemba Mosi mwaka 2026 na yanahusu pikipiki, bodaboda na bajaji pekee, huku akiwataka madereva na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ili kulinda maisha.