Zenj FM
Zenj FM
13 October 2026, 22:29

Mkurugenzi Mkuu wa ZHSF, Heri Marwa, atoa siku saba kwa kampuni zinazofanya kazi Zanzibar kuhakikisha zinasajili wafanyakazi wao na kuwasilisha michango ya bima ya afya kwa mujibu wa sheria. Je, ni hatua gani zitachukuliwa dhidi ya kampuni zitakazoshindwa kutekeleza agizo hilo?
Na Mary Julius.
Mfuko wa Huduma ya Bima ya Afya Zanzibar (ZHSF) umezipa siku saba kampuni zinazofanya kazi Zanzibar kuhakikisha zinasajili wafanyakazi wao na kuwasilisha michango ya bima ya afya kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa ofisi za ZHSF Michezani Mall, wilaya ya Mjini Zanzibar, Mkurugenzi Mkuu wa ZHSF, Heri Marwa, amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki yao ya huduma za bima ya afya, huku waajiri wakitimiza wajibu wao wa kisheria.
Amesema hadi Septemba 2026, sekta binafsi ilikuwa na wachangiaji 91,817, huku jumla ya wanachama pamoja na wategemezi wao ikifikia 241,000.
Aidha, amesema kati ya kampuni 138 zilizoitikia wito wa usajili, kampuni 52 zimekamilisha taratibu hizo, huku kampuni 86 zikiendelea na mchakato wa usajili.
Mkurugenzi Heri amezitaja ambazo bado hazijakamilisha usajili wa wafanyakazi wao ni Iris Construction, CRJE Jiangxi, United Ram Construction Limited na Til Construction.
Katika hatua nyingine, Marwa amesema ZHSF itaanzisha utaratibu wa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali ili kutafuta suluhisho la muda mrefu kwa kampuni ambazo zimekuwa zikisita kujiandikisha na mfuko huo.
Amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha utekelezaji wa sheria na kuhakikisha waajiri wote wanatimiza wajibu wao wa kusajili wafanyakazi na kuwasilisha michango ya bima ya afya.