Zenj FM

Zoezi la usafi Mwembe shauri,Diwani awaonya wazazi kuwatuma watoto kutupa taka

16 November 2026, 22:42

Sheha wa Mwembe Shauri Abdallah Ali akifanya usafi na wananchi wa shehia hiyo katika maeneo ya Mkungu malofa ikiwa ni katika uzinduzi wa zoezi la ufanyaji wa usafi katika shehia zote za Unguja na Pemba.

Diwani wa Raha Leo, Ismail Malik Mohammed, amewataka wazazi kuacha kuwapa watoto wadogo taka za kwenda kutupa jalalani, akisema tabia hiyo inachangia kutapakaa kwa taka na kuchafua mazingira. Wito huo umetolewa wakati wa zoezi la usafi la siku 15 katika Shehia ya Mwembe Shauri, linalolenga kuimarisha usafi na kujiandaa na mvua zinazotarajiwa kunyesha pamoja na mapokezi ya wageni kuelekea AFCON.

Na Mary Julius.

Diwani wa Raha Leo, Ismail Malik Mohammed, amewataka wazazi kuacha kuwapa watoto wadogo taka za kwenda kutupa katika majaa, ambapo amesema  tabia hiyo inachangia kutapakaa kwa taka na kuchafua mazingira ya makazi.

Akizungumza na Zenji FM wakati wa zoezi la usafi katika Shehia ya Mwembe Shauri, amesema wazazi wanapaswa kuhakikisha taka zinafikishwa kwenye maeneo maalumu badala ya kuwaachia watoto ambao hawana uwezo wa kuzibeba.

Sauti yta Ismail Malik Mohammed

Amesema zoezi hilo la siku 15 llinalenga kujiandaa na mvua zinazotarajiwa kunyesha, kudhibiti athari za mafuriko na kuifanya Zanzibar kuwa safi kuelekea AFCON na mapokezi ya wageni.

Aidha, amesema wananchi wana wajibu wa kutunza mazingira na kulinda miundombinu iliyojengwa na Serikali ya awamu ya nane chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ikiwemo barabara, elimu na afya.

Sauti ya Ismail Malik Mohammed,

Kwa upande wake, Sheha wa Mwembe Shauri Abdallah Ali amesema shehia itaongeza vifaa vya usafi na kamati itapita nyumba kwa nyumba kukagua hali ya usafi, huku akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokiuka wajibu huo.

Aidha  ameeleza umuhimu wa kuunda kikundi cha wakusanyaji taka ili kudhibiti utupaji ovyo na kuimarisha usafi katika shehia hiyo.

Sauti ya Sheha wa Mwembe Shauri Abdallah Ali

Naye mwananchi wa shehia hiyo, Omar Makame, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza zoezi hilo kwa mshikamano na ushirikiano kati ya viongozi na wananchi.

Sauti ya Omar Makame

Kwa upande wake, Amina Mwadini amewahimiza wananchi kujitolea kufanya usafi kila siku na kuwataka wazazi kutowapa watoto wadogo taka ambazo hawawezi kuzibeba, ili kuzuia uchafuzi wa mazingira.

Sauti ya Amina Mwadini