Zenj FM

Mandoba aigusa familia iliyoathiriwa na moto kwa msaada wa mabati 50

17 June 2026, 16:13

Mwakilishi wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Magharibi, Fatma Ramadhan Mandoba, akimkabidhi Asha Kombo Khamis,mabati hamsini.

Mwakilishi wa Viti Maalumu Mkoa wa Magharibi, Fatma Ramadhan Mandoba, ametoa mabati 50 kwa familia iliyopoteza nyumba kutokana na moto katika Jimbo la Dimani. Amesema msaada huo ni sehemu ya kuonesha mshikamano na kuwahimiza viongozi wengine kujitokeza kusaidia familia hiyo kupata makazi ya kudumu.

Na Mariam Seif .

Mwakilishi wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Magharibi, Fatma Ramadhan Mandoba, ametoa msaada wa mabati 50 kwa familia iliyopoteza makazi yake kufuatia kuungua kwa nyumba katika Jimbo la Dimani.

Msaada huo umetolewa wakati wa ziara yake katika Jimbo la Dimani kwa lengo la kuonesha mshikamano na ushirikiano wa viongozi kwa wananchi wao. Nyumba ya familia hiyo iliteketea kwa moto usiku wa kuamkia tarehe 12 Juni, 2026, na kuwaacha wakikabiliwa na changamoto ya makazi.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Mandoba amesema kuwa ni wajibu wa viongozi kusimama pamoja na wananchi wakati wa matatizo, huku akitoa wito kwa viongozi wengine wa chama pamoja na wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia ili familia hiyo iweze kurejeshewa makazi ya kudumu haraka iwezekanavyo.

Sautinya Fatma Ramadhan Mandoba.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Wilaya ya Dimani, Subira Ali Mzee, ameitaka familia hiyo kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu wanachokipitia. Amesema kuwa uongozi utaendelea kushirikiana nao hadi watakapopata makazi yao kama ilivyokuwa awali.

Sauti ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Wilaya ya Dimani, Subira Ali Mzee

Naye mama aliyepata athari za tukio hilo, Asha Kombo Khamis, ameushukuru uongozi pamoja na watu wote waliomsaidia na kumuunga mkono katika kipindi hicho kigumu.

Sauti ya Asha Kombo Khamis.