Zenj FM

Wanaoiba pikipiki mikononi mwa Polisi mkoa wa Kusini Unguja

8 May 2024, 3:03 pm

Kamanda wa Polisi Mkoa wa kusini unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Daniel Shillah akizungumza na waandishi wa habari Tunguu.

Na Mary Julius.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za wizi wa pikipiki katika maeneo ya mikusanyiko ya watu ikiwemo kwenye harusi, misiba na nyumba za ibada.

Akizungumza na waandishi wa habari huko Tunguu Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kusini Unguja Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Daniel Shillah amewataja watuhumiwa hao ni Iddi Abdalla Kisumba M. 20 na Rashid Abdalla Sadala M. 19 wakaazi wa Kidimni, Fakih Kassim Khamis M.19 mkaazi wa Amani na Ahmed Amour Abdalla M 24 Mkaazi wa Makunduchi, ambao wamekamatwa katika maeneo tofauti wakiwa wameshaiba pikipiki tatu.

Aidha Kamanda shillah amesema wamefanikiwa kuwakamata watu wengine watatu ambao wanajihusisha na unyanganyi wa kutumia silaha kwa kuwavizia watembea kwa miguu huwatishia kwa mapanga na kuwapora kisha kukimbia kwa kutumia pikipiki, akiwemo Khalid Salum Said M. 20 Mkaazi wa Fuoni, Yassir Abdalla Shaaban M 30 Mkaazi wa Fuoni na Ali Mohamed Ali (Shetani Kiro) M. 28 Mkaazi wa Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja.

Sauti ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa kusini unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Daniel Shillah

Katika hatua nyingine SACP Shillah amesema Jeshi la Polisi kwa kupitia doria na misako limefanikiwa kuwakamata (1) Ameir Abdalla Abdalla miaka 33 Mkazi wa Paje (0) Hamza Ali Balongo miaka 49 Mshirazi Mkazi wa Paje (iii) Ahmed Amour ABDALLA miaka 24 Mshirazi Mkazi wa Makunduchi kwa tuhuma za kuvunja nyumba na kuiba katika maeneo ya Paje, Bwejuu ni Michanvi katika msako huo watuhumiwa wamepatikana na mali walizoiba ikiwemo TV moja aina ya LG inch 50 iliyoibiwa kwenye ofisi za Chama cha Mapinduzi Tawi la Paje, TV moja inchi 16 na taa moja, simu mbili Samsung 522 na Iphone 12, power bank moja mali za watalii.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Daniel Shillah akionyesha tv iliyoibiwa.