Zenj FM
Zenj FM
24 June 2026, 22:04

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, ameagiza kufungwa kwa baa tatu katika eneo la Kambodia, Kizimkazi Mkunguni, baada ya kubainika kukiuka sheria na taratibu za uendeshaji pamoja na kusababisha kero ya kelele karibu na skuli. Hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wananchi, huku Serikali ikiwataka wamiliki wa biashara kufuata sheria ili kuepuka hatua za kisheria.
Na Mwandishi wetu.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, ameiagiza Bodi ya Vileo, Baraza la Sanaa na Sensa ya Filamu pamoja na Baraza la Mji Kusini kuzifungia na kuzichukulia hatua baa tatu zilizopo eneo la Kambodia, Shehia ya Kizimkazi Mkunguni, kwa kukiuka sheria na taratibu za uendeshaji wa shughuli hizo.
Agizo hilo limetolewa baada ya Mkuu huyo wa Mkoa kufanya ziara ya kushtukiza kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi wa Shehia za Kizimkazi Mkunguni, Dimbani na Kibuteni wakati wa mkutano wa hadhara. Wananchi hao walilalamikia kelele za muziki kutoka katika baa hizo zinazopatikana karibu na shule ya Kizimkazi Mkunguni, hali inayosababisha usumbufu kwa wanafunzi, walimu na jamii inayowazunguka.
Hamida amesema baada ya kupokea malalamiko hayo aliamua kuchukua hatua za haraka kwa kufika katika maeneo hayo na kubaini kuwa baadhi ya shughuli zilikuwa zinaendeshwa bila vibali vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Baraza la Mji Kusini, Mussa Haji, amesema hatua ya kufunga baa hizo ni kielelezo cha kutovumiliwa kwa ukiukwaji wa sheria na pia ni fundisho kwa wamiliki wengine wa biashara.
Amehimiza wawekezaji na wamiliki wa maeneo ya biashara kufuata sheria na taratibu zote za Serikali ili kuepusha usumbufu na hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao.
Naye baadhi ya wamiliki wa baa hizo wamesema wako tayari kushirikiana na mamlaka husika kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa ili kuhalalisha shughuli zao za biashara.
Baa zilizofungiwa ni pamoja na New Maisha Pub, Bar Mpya na baa nyingine iliyobainika kukiuka masharti ya uendeshaji yaliyowekwa na mamlaka husika.