Zenj FM
Zenj FM
1 June 2026, 17:10

Wafanyabiashara na wajasiriamali wa Wilaya ya Kati wametakiwa kujiunga katika vikundi ili kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kuimarisha biashara zao. Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa Kati, Dkt. Mwanaisha Ali Said, wakati wa mkutano wa wafanyabiashara wa Soko la Dunga.
Na Hakika Mwinyi.
Wafanyabiashara na wajasiriamali wa Wilaya ya Kati wametakiwa kujiunga katika vikundi na kujisajili rasmi ili waweze kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu kwa lengo la kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Kati, Dkt. Mwanaisha Ali Said, katika mkutano wa wafanyabiashara wa Soko la Dunga uliofanyika katika ukumbi wa Manispaa Kati. Amesema mkutano huo umeandaliwa kujadili changamoto za soko na kutafuta suluhisho la pamoja kwa maendeleo ya wafanyabiashara.
Dkt. Mwanaisha pia amewahimiza wafanyabiashara kuzingatia usafi wa soko, kulipa ada kwa wakati na kufanya biashara katika maeneo rasmi waliopangiwa ili kudumisha mazingira bora ya biashara.
Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Manispaa Kati, Said Hassan Shaaban, amesema changamoto za kutokuelewana kati ya manispaa na wafanyabiashara zimeanza kupatiwa ufumbuzi kupitia mazungumzo na ushirikiano.
Naye Yussuf Issa Ali, akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara, ameahidi kuwa watafuata maelekezo waliyopewa ikiwemo kuimarisha usafi na kuendesha biashara zao katika maeneo rasmi.
Mkutano huo umewakutanisha viongozi wa Manispaa Kati na wafanyabiashara wa Soko la Dunga kwa lengo la kujadili changamoto na kuimarisha mazingira ya biashara.