Zenj FM

PBZ yaweka rekodi mpya, yatoa gawio la bilioni 15.3 kwa SMZ

20 June 2026, 15:06

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Juma Malik Akil,akipokea mfano wa hundi ya gawio kutoka Bank ya Watu wa Zaznibar PBZ hafla iliyo fanyika katika ukumbi wa makao makuu ya banki hiyo Mpirani Wilaya ya Mjini Zanzibar

Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) imekabidhi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar gawio la zaidi ya shilingi bilioni 15.3, ikiwa ni ongezeko la asilimia 53 ikilinganishwa na mwaka uliopita. Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Juma Malik Akil, amepongeza mafanikio hayo akieleza kuwa yanatokana na ufanisi wa kazi, matumizi ya teknolojia na kuongezeka kwa wateja.

Na Mary Julius.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Juma Malik Akil, amepongeza utendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar baada ya benki hiyo kuendelea kuimarika na kuongeza mchango wake kwa uchumi wa Zanzibar.

Waziri Akil ametoa pongezi hizo wakati wa hafla ya kupokea gawio la mwaka huu kutoka PBZ, ambapo benki hiyo imekabidhi zaidi ya shilingi bilioni 15.3 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 53 ikilinganishwa na gawio la mwaka uliopita.

Akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wajumbe wa bodi ya wakurugenzi, menejimenti ya benki na serikali kama mbia mkuu, Waziri amesema ameridhishwa na mwenendo wa PBZ ambao umeendelea kutoa gawio kila mwaka, jambo linaloonyesha uimara wa benki hiyo na usimamizi mzuri wa rasilimali zake.

Amesema mafanikio hayo yametokana na kuongezeka kwa ufanisi wa kazi, matumizi ya mifumo ya kisasa ya kidijitali, udhibiti wa matumizi yasiyo ya lazima pamoja na ongezeko la wateja wanaotumia huduma za benki hiyo.

Waziri Akil ameipongeza bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya PBZ kwa juhudi zao za kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo, akieleza kuwa gawio hilo ni sehemu muhimu ya mapato ya ndani yatakayosaidia utekelezaji wa miradi na mipango ya maendeleo ya serikali.

Sauti ya Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Juma Malik Akil.

Aidha, ameitaka Hazina kuhakikisha mashirika na taasisi nyingine za umma zinaongeza ufanisi na kuiga mfano wa PBZ kwa kutoa gawio kwa serikali kila mwaka, ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya uchumi wa Zanzibar.

Waziri Akil, amesema serikali itaendelea kufuatilia utendaji wa mashirika ya umma na kuchukua hatua stahiki kwa yale ambayo hayafikii malengo yaliyowekwa, huku ikihimiza uwajibikaji na tija katika matumizi ya rasilimali za umma.

Sauti ya Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Juma Malik Akil.