Zenj FM
Zenj FM
8 May 2026, 14:04

Taasisi ya Zanzibar International Development Organization (ZIDO) imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 30 kwa watoto yatima na watu wenye ulemavu huko Dunga. Msaada huo umejumuisha vifaa vya skuli, visaidizi mwendo pamoja na mbuzi kwa familia za watu wenye ualbino ili kuwawezesha kiuchumi na kijamii.
Na Mary Julius.
Taasisi ya Zanzibar International Development Organization (ZIDO) imesema itaendelea na juhudi za kukuza na kuimarisha ustawi wa Wananchi hasa watoto yatima na makundi ya watu wenye ulemavu nchini.
Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Ramadhan Makame Mbanja ametoa kauli hiyo huko Dunga wakati akikabidhi mbalimbali kwa watoto yatima, watu wenye ulamavu wa viungo na ngozi.
Amesema Taasisi hiyo imekuwa ikizingatia kwa karibu makundi hayo kwa kuyasaidia mahitaji ili kuona na wao wanajiona sawa na watu wengine katika jamii na wanastahili kupata haki zote za msingi.
Amesema vifaa hivyo vilivyogharimu jumla ya shilingi milioni thalathini vitawarahisishia katika shughuli zao mbalimbali za kiuchumi, kielimu na kimaisha hivyo ameziomba taasisi nyengine na watu wenye uwezo kuendelea kuwasaidia watu hao.
Afisa ulemavu Wilaya ya Kati Abdalla Aladi amesema utolewaji wa vifaa hivyo kwa watu wa makundi hayo unatoa faraja na furaha katika kutimiza ndoto zao za maisha huku akiwahimiza wazazi wenye watoto wenye ulemavu kutowaficha majumbani na badala yake kwenda kuwaorodhesha wilayani ili waweze kutambulika na kupatiwa haki zao za msingi.
Nao kwa upande wao Katibu wa Taasisi ya watu wenye ualbino Zanzibar Mohd Ali Mohd na wananchi waliopatiwa msaada huo Mwanakombo Mohammed na Ali Mzee wameelezea kufurahishwa kwao na misaada hiyo waliopatiwa kwani itawasaidia kurahisisha shughuli zao ikiwemo za malezi pamoja na kujiwezesha kiuchumi.
Msaada uliotolewa na Jumuiya hiyo ni pamoja na vifaa vya skuli kwa watoto yatima 40, visaidizi mwendo 40 kwa watoto wenye ulemavu wa viungo na mbuzi 100 kwa familia kumi na tano kwa ajili ya kufuga watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) ambavyo vimegharimu jumla ya shilingi milioni thalathini