Zenj FM

Magharibi B yatikisa takwimu za talaka Zanzibar

25 November 2026, 13:36

Mtakwimu wa Divisheni ya Takwimu za Vizazi na Vifo, Haji Vuai Ali.

Takwimu mpya za OCGS zaonesha Wilaya ya Magharibi B kuongoza kwa talaka Zanzibar baada ya kurekodi talaka 36 kati ya 79 katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2026. Licha ya Magharibi B kuongoza, idadi ya talaka Zanzibar imepungua kwa asilimia 57.1 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Na Ivan Mapunda.

Wilaya ya Magharibi B imeongoza kwa idadi ya talaka Zanzibar baada ya kurekodi talaka 36 kati ya 79 zilizosajiliwa katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu, sawa na asilimia 45.6 ya talaka zote katika robo hiyo.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa wilaya hiyo inaongoza kwa talaka zilizorekodiwa, ikifuatiwa na Mjini iliyokuwa na talaka 18 na Mkoani iliyorekodi 14.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), iliyotolewa na Mtakwimu wa Divisheni ya Takwimu za Vizazi na Vifo, Haji Vuai Ali, idadi ya talaka imepungua kwa asilimia 57.1 ikilinganishwa na talaka 184 zilizorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2025.

Amesema Septemba ilikuwa na idadi kubwa zaidi ya talaka 36, ikifuatiwa na Agosti 32 na Julai 11.

Amefafanua kuwa Magharibi B ilirekodi ongezeko la talaka kutoka sita Julai hadi 14 Agosti na kufikia 16 Septemba.

Katika wilaya nyingine, Magharibi A ilirekodi talaka sita, Kaskazini B tatu na Kati mbili. Wilaya za Kaskazini A, Kusini Unguja, Micheweni, Wete na Chake Chake hazikurekodi talaka katika kipindi hicho.

Wakati talaka zikipungua, usajili wa ndoa nao umeshuka kwa kiwango kikubwa. Taarifa hiyo inaonesha kuwa ndoa 176 zilisajiliwa katika robo hiyo, ikiwa ni punguzo la asilimia 89.4 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.

Magharibi B iliongoza kwa usajili wa ndoa 44, ikifuatiwa na Mjini iliyokuwa na 39, huku Mkoani ikirekodi ndoa tatu pekee.

Sauti ya Mtakwimu wa Divisheni ya Takwimu za Vizazi na Vifo, Haji Vuai Ali.

Katika upande wa vizazi, watoto 7,693 walisajiliwa kuwa vizazi hai, wakiwamo wavulana 3,879 na wasichana 3,814. Idadi hiyo imepungua kwa asilimia 59.9 ikilinganishwa na watoto 19,168 waliosajiliwa katika robo kama hiyo mwaka 2025.

Magharibi B pia iliongoza kwa vizazi hai 1,163, ikifuatiwa na Mjini yenye watoto 1,090, wakati Kaskazini B ilirekodi idadi ndogo zaidi ya watoto 174.

Aidha, jumla ya vifo 526 vilisajiliwa, ambapo wanaume walikuwa 328 na wanawake 198. Wilaya ya Mjini iliongoza kwa vifo 110, huku Kusini ikiwa na idadi ndogo zaidi ya 13.

Sauti ya Mtakwimu wa Divisheni ya Takwimu za Vizazi na Vifo, Haji Vuai Ali.