Moravian Mbeya yaimarisha taasisi zake za elimu,wanachuo 44 wahitimu fani ya ualimu
18 April 2024, 18:59
Katika kuthamini na kuunga jitihada za Serikali katika Sekta ya elimu nchini,kanisa la Moravian Jimbo la kusini magharibi limeendelea kuimarisha uendeshaji wa taasisi zake za elimu ikiwemo Shule,vyuo vya ufundi na ualimu kuhahakisha vinazalisha wasomi wengi ambao watakuwa msaada kwenye jamii kupitia fani wanazosomea.
Na Hobokela Lwinga
Chuo cha ualimu Mbeya Moravian cha kanisa la Moravian Tanzania jimbo la kusini magharibi kimefanya mahafali ya 15 ambapo wanafunzi 44 wamehitimu.
Sherehe za mahafali hiyo zimefanyika katika ukumbi wa chuo cha ufundi Moravian kadege Mbeya zimepambwa na burudani mbalimbali kutoka wanafunzi wahitimu na imehudhuriwa na mamia ya wazazi na wageni waalikwa,mgeni wa heshima akiwa ni Katibu Mkuu wa kanisa la Moravian Tanzania jimbo la kusini magharibi Israel Mwakilasa.
Akizungumza katika mahafali hiyo mgeni wa heshima ndugu Israel Mwakilasa amesema vyuo vingi kushindwa kujiendesha inasababishwa na sera na mitaala inayobadilishwa kwani wanafunzi wengi wanashindwa kufikia vigezo ikiwemo ufaulu wao.
Aidha Katibu Mkuu huyo Mwakilasa amewataka wahitimu hao kuheshimu na kutunza asili yao na asili ya taifa lao.
Hata hivyo mkuu wa chuo Mch.Alfred Mkondya amesema chuo Kimefanikiwa kutoa elimu kwa Wanafunzi hali iliyosabisha wanafunzi wengi kufanya vizuri kwenye mitihani kutokana na uwepo wa Wakufunzi wenye weledi wa kufundisha.
Baadhi ya wazazi wa watoto wahitimu wamewataka wahitimu hao kuzingatia yale yote waliyofundishwa na wakufunzi wao huku akiwataka Wahitimu kumtegemea Mungu.
Kupitia risala iliyowakilishwa na mhitimu ambaye ni Rais wa chuo hicho Trifa Sanga imetoa shukrani kwa uongozi wa chuo na kanisa kwa kuweka mazingira rafiki kwa Wanafunzi sambamba na hayo imeeleza changamoto kadhaa zinazozikabili chuo ikiwemo ukosefu wa maktaba na viwanja michezo na ukosefu wa hosteli za wanafunzi wa kiume.