Nuru FM
Nuru FM
3 April 2026, 09:37

Nauli imepanda jambo lililopelekea baadhi ya abiria kuiomba mamlaka husika kutangaza bei halisi.
Na Telesia Chalamila
Baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kutangaza ongezeko la bei ya mafuta, madereva wa vyombo vya usafiri wa uma Manispaa ya Iringa wameamua kupandisha bei ya nauli.
Wakizungumza na Nuru FM baadhi ya madereva bajaji manispaa ya Iringa wamesema kuwa wameamua kupandisha bei ya nauli kutoka sh. 800 hadi 1000 hali inayozua hofu ya kupoteza wateja.
Kwa upande wao baadhi ya madereva wa daladala Manispaa ya Iringa wameiomba serikali kutazama upya bei za nauli ambazo kwao bado hawajapandisha.
Nao baadhi ya Abiria kutoka Kituo cha Miyomboni Iringa mjini wamedai kuwa ongezeko la nauli kutokana tangazo la bei ya mafuta na kupanda kwa bei za bidhaa za vyakula limezidi kuwa mzigo mkubwa kwao.
Ewura imetangaza bei mpya ya mafuta jumatano aprili 1 2026 ambapo kwa manispaa ya iringa mjini mafuta yalikuwa yakiuzwa shilingi 2877 na sasa yamepanda mpaka shilingi 3920.