Nuru FM

CAMFED watoa mafunzo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

5 April 2025, 7:18 am

Wasichana wakiwa katika Mafunzo. Picha na Adelphina Kutika

Na Adelphina Kutika

Wasichana waliopokea msaada kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Campaign for Female Education (CAMFED) wameiomba Serikali kuhakikisha wakulima wote nchini wanapata mbolea ya ruzuku kwa wakati, ili kuwasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao na kufikia malengo ya Serikali ya kukuza sekta ya kilimo na kuboresha kipato cha wakulima.

Hayo yamebainishwa na mkufunzi wa kilimo wa mkoa wa Iringa, Irene Mubito, katika mafunzo ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi yaliyodumu kwa takribani siku 10 Katika Sekondari ya Kilolo, iliyopo Halmashauri ya Kilolo.

Mubito amesema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, hivyo ni muhimu Serikali itoe msaada wa mbolea ya ruzuku kwa wasichana hao wanaojihusisha na kilimo ili waweze kufanya kazi zao bila kutegemea mvua pekee.

“Wasichana hawa wanajifunza mbinu mbalimbali kutoka kwa wataalamu wa kilimo, ili waweze kuzitumia katika kilimo cha kisasa na kinachozingatia mabadiliko ya tabia ya nchi,” amesema Mubito.

Kwa upande mwingine, Hapinass Mkini, mwezeshaji wa programu ya kilimo wilaya ya Iringa, amesema kuwa wanajivunia mafanikio ya mafunzo hayo kwani yamekuwa na athari chanya kwa jamii.

“Tunajivunia kuona kwamba washiriki wa mafunzo haya wameweza kutunga mikakati ya kusaidia jamii zao, na sasa wanashiriki katika kutoa elimu ya kilimo kwa wakulima wengine katika maeneo yao,” alisema Mkini.

Wanufaika wa mafunzo hayo, Shukran Agustino na Agnes James Mmewa, wameshukuru shirika la CAMFED kwa kuwawezesha kupata elimu ya kilimo inayozingatia mabadiliko ya tabia ya nchi, na kusema kuwa elimu hiyo itawasaidia kulima kwa ufanisi zaidi na kutumia dawa bora kwa mifugo yao.

Aidha, tutatumia mbinu bora za udhibiti wa magonjwa kwa mifugo, jambo litakaloongeza uzalishaji na mapato yetu,” alisema Shukran Agustino.

Hata hivyo Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za CAMFED kuendeleza wanawake na wasichana katika sekta ya kilimo, ili kuweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi na kuhakikisha usalama wa chakula na maisha bora kwa jamii.